Boniface Mwangi - Uhuru nyamaza na ujipange kuenda nyumbani, unaharibia Raila, Karua kura

Rais Uhuru Kenyatta na mwanaharakati Boniface Mwangi
Rais Uhuru Kenyatta na mwanaharakati Boniface Mwangi
Image: Facebook

Aliyekuwa mwanahabari mpiga picha na mwanaharakati wa haki za kibinadamu Boniface Mwangi sasa anawataka wandani wa rais Uhuru Kenyatta kumkanya dhidi ya kumpigia debe mgombea urais wa muungano wa Azimio la   Umoja-One Kenya, Raila Odinga na mgombea mwenza Martha Karua kwa kile alisema anawaharibia kura nyingi na kuwapotezea ufuasi.

Kupitia kwenye ukurasa wake wa Facebook, Mwangi alimtaka rais Kenyatta kukaa kimya kuhusiana na chochote kinachoendelea na siasa nchini na badala yake kuanza kujiandaa kuenda nyumbani. Mwangi alisema sauti ya Uhuru Kenyatta hahitajiki kwa sababu kila anapofungua mdomo wake kuongeac anapotezea Raila Odinga kura nyingi.

“Kwa wanaomfanyia kazi Rais Uhuru Kenyatta mwambieni anyamaze aanze kujiandaa kwenda nyumbani. Sauti yake haihitajiki katika kampeni hii,” Mwangi alisema.

Aidha mwanaharakati huyo ambaye kwa sasa anampigia upato Raila kuelekea uchaguzi wa Agosti kwa sababu ya uswahiba wake na mgombea mwenza Martha Karua alidai raia Kenyatta na naibu wake William Ruto ndio wamekuwa wafisadi wakubwa na haina haja kuanza kujionesha kwamab anafanya kazi zikiwa zimesalia wiki tatu tu kutamatika kwa awamu ya uongozi wake.

“Hakupigana na ufisadi, yeye na Ruto waliuwezesha. Anawaumiza Raila na Martha kwa kuwaunga mkono. Uhuru na Ruto ndio tatizo! Utawala wa Uhuruto ndio utawala fisadi zaidi katika historia ya nchi yetu. Uhuru Kenyatta kujifanya kufanya kazi wiki tatu zilizopita kabla ya muhula wake kwisha ni kujifanya tu,” Mwangi alifoka kwa hasira.

Mwanaharakati huyo mwenye misimamo mikali asiyetetereka alisema kwa mwongo mmoja sasa serikali ya Jubilee imekuwa ikimaza damu kazini na kuwekeza nguvu nyingi katika kunyakua mali ya umma na ni wakati wamalize waende nyumbani kimya kimya badala ya kujiingiza katika siasa na kuwapata tope wenzao wanaowania.

“Miaka 10 iliyopita imekuwa mbaya sana kwa Wakenya. Ufisadi mbaya sana. Uhuru na Ruto waliendelea kufanya karamu na kupata mishahara mikubwa huku sisi tukiteseka. UhuruTo lazima turudi nyumbani pamoja! Wamalize waende,” Mwangi alisema.

Boniface Mwangi kwa muda mrefu amekuwa akitofautiana na viongozi wengi wa siasa akiwemo Raila Odinga lakini pindi tu baada ya Rafiki wake wa karibu Martha Karua alipoteuliwa kama mgombea mwenza wa Raila, Mwangi alibadilisha fikira zake na kuanza kumpigia debe.