Seneta wa Kajiado amtema Ruto na kumuidhinisha Raila

Mpaayei sasa ameapa kuunga mkono hoja ya Azimio na viongozi wake.

Muhtasari

•Huku akijiunga na Azimio, Seneta huyo alidai kwambalitendewa dhuluma katika chama chake cha awali cha UDA.

•Gavana Ole Lenku alisema uungwaji mkono wa Mpaayei utaipa nguvu kambi ya Raila tunapoelekea kwenye uchaguzi.

akimkaribisha Seneta Philip Mpaayei kwa Azimio Jumatano Julai 13, 2022.
Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku akimkaribisha Seneta Philip Mpaayei kwa Azimio Jumatano Julai 13, 2022.
Image: FACEBOOK// JOSEPH OLE LENKU

Seneta wa Kaunti ya Kajiado Philip Mpaayei amegura kambi ya Naibu Rais William Ruto na kuhamia kambi ya mgombea urais wa Azimio-One Kenya Raila Odinga.

Mpaayei alipokelewa katika nyumba yake mpya na Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku mnamo Jumatano.

Huku akijiunga na Azimio, Seneta huyo alidai kwambalitendewa dhuluma katika chama chake cha awali cha UDA.

Wakati huo huo alidai kuwa aliibiwa wakati wa kura ya mchujo ya chama iliyofanyika mwezi Aprili.

"Ukweli sasa umenidhihirikia. UDA ilinichuja kiujanja na kuweka mgombea useneta dhaifu ambaye atabanduliwa na mgombea wa Azimio," Mpaayei alisema.

Aliongeza "Muungano wa Kenya Kwanza ni pango la watapeli wa kisiasa ambao hawatambui demokrasia na matakwa ya wananchi. Timu hiyo ni muungano wa watu wenye ubinafsi wanaohatarisha haki na hilo lilidhihirika kupitia wizi wao wa kura za mchujo za chama".

Huku akimkaribisha katika Azimio, gavana Lenku alisema uungwaji mkono wake utaipa nguvu kambi ya Raila tunapoelekea kwenye uchaguzi.

"Nashukuru kwa mapambazuko mapya huko Kajiado kufuatia uamuzi wa Seneta Philip Mpaayei, aliyekuwa wa Chama cha UDA, kujiunga rasmi na mrengo wangu wa kisiasa. Asante Seneta Mpaayei kwa kurudi nyumbani! Pamoja Tutashida!" Lenku alisema kupitia Facebook.

Mpaayei alishinda kiti cha useneta wa Kajiado katika uchaguzi wa 2017 kupitia tikiti ya Jubilee lakini baadae akaondoka na kujiunga na chama cha UDA.

Seneta huyo hata hivyo alipoteza kura za mchujo mwezi Aprili kwa mgombea wa sasa wa UDA, Kanar Seki.

Mpaayei sasa ameapa kuunga mkono hoja ya Azimio na viongozi wake.

“Sasa nataka kusema nimejiunga na muungano wa Azimio la Umoja, nilijiondoa rasmi katika chama cha UDA na sitamuunga mkono kiongozi yeyote anayeshirikiana nacho,” alisema.