Siaya: Rasanga ampigia debe seneta Orengo kumrithi kama gavana

Rasanga anaondoka baada ya kudumu kama gavana wa Siaya kwa miaka kumi.

Muhtasari

• "Mpige kura zenu kwa mtu anayefahamu vizuri shida ya Wananchi," - Rasanga.

• Seneta Orengo alikabidhiwa tikiti ya moja kwa moja ya ODM kuwania ugavana.

gavana wa siaya
gavana wa siaya
Image: Hisani: The Star

Gavana wa Kaunti ya Siaya  Cornel Rasanga amempigia debe Seneta wa kaunti hiyo James Orengo  kuwa mrithi wake katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Mwanasiasa huyo aliweka haya wazi wakati wa kongamano lililowaleta pamoja viongozi wa chama hicho katika kaunti ya Siaya na Walimu  wa Chekechea. Mkutano huu ulifanyika katika eneo bunge la Ugunja.

''Niliamua kupanga hafla hii ili niongee nanyi kwa mara ya mwisho, na pia kuwahakikishia kwamba singependa kuacha kaunti ya Siaya katika Mikono ya watu walaghai'' Rasanga alisema.

Kwa muda Rasanga ameonekana kukaa kimya kuhusu siasa za kaunti ya Siaya haswa kuhusu pendekezo la yule ambaye angependa kuchukua uongozi wa Siaya baada ya kipindi chake cha mihula miwili kutamatika. 

IEBC iliwaidhinisha wagombea wengine watatu kuwania nyadhifa hiyo ya juu zaidi katika uongozi wa kaunti ambao ni pamoja na Nicholas Gumbo wa UDM, William Ochieng anayewania kama mgombea huru na Millicent Oduor wa UDA.

'' Venye mlinichangua  kwa vishindo kuwa mwakilishi wenu, naamini kuwa vivyo hivyo mchague James Orengo kama gavana mnamo Agosti 9,''  Rasanga alisema.

Gavana Rasanga alizidi kumpigia Orengo debe kwa kusema kuwa yeye si mwanasiasa tu, bali  pia alichangia sana katika kupigania uhuru wa nchi hii.

''Mchango wa Orengo hauonekani tu hapa  Siaya, pia alikuwa  katika mstari wa mbele wa ukombozi wa pili  wa nchii hii  na anaelewa siasa ya hapa nchini'' Rasanga alisema.

Rasanga alichaguliwa kwa mara ya kwanza kama gavana mwaka wa 2013 kupitia tikiti ya chama cha ODM baada ya kumbwaga Oduol katika kinyang'anyiro hicho kilichoshuhudia ushindani mkali.

Mnamo 2017 alishinda kiti cha ugavana tena akiwashinda mbunge wa Rarieda kipindi hicho,  Nicholas Gumbo.