Mahakama yabatilisha uamuzi wa NCIC kuharamisha 'Hatupangwingwi' na 'Watajua hawajui'

NCIC ilitoa orodha ya maneno yasiyofaa kutumika katika kampeni mnamo Aprili mwaka huu.

Muhtasari

• Jana, mahakama kuu ilibatilisha uamuzi wa NCIC kupiga marufuku maneno ya hatupangwingwi na Watajua Hawajui.

• Hii ni baada ya chama cha mawakili kuelekea mahakamani Aprili baada ya NCIC kuharamisha maneno hayo.

Mwenyekiti wa NCIC Samwel Kobia na naibu rais William Ruto
Mwenyekiti wa NCIC Samwel Kobia na naibu rais William Ruto
Image: Maktaba

Ni afueni kwa mrengo wa naibu rais William Ruto, Kenya Kwanza baada ya mahakama ya juu kutupilia mbali matakwa ya tume ya uwiano na utangamano NCIC ya kutaka maneno kama Sipangwingwi na Watajua Hawajui kuharamishwac katika kutumiwa na wanasiasa katika kampeni zao.

Maneno haya yalikuwa yanatumiwa sana na mrengo wa naibu rais huku akizidi mbele hadi kufanya ‘remix’ na wimbo wa Sipangwingwi na msanii wa gengetone Exray na kuutumia kama wimbo rasmi katika kampeni zake kabla ya NCIC kuharamisha neno hilo kwa madai kwamba huenda likawa na maana ya uchochezi.

Mapema mwezi April mwaka huu, NCIC iliachia orodha ya maneno kadhaa ambayo iliharamisha kutotumika na wanasiasa katika hafla za kampeni lakini mawakili walielekea mahakamani kupinga marufuku hiyo Alhamis Jaji wa mahakama kuu Anthony Ndung’u alitaja kesi hiyo na kusema kwamba NCIC ikiongozwa na mchungaji Samwel Kobia haikufuata njia zac kisheria katika kuharamisha maneno hayo.

“Amri inatolewa kwa hivyo kubatilisha uamuzi wa NCIC uliotolewa Aprili 8, 2022, kuhusu kamusi ya maneno ya chuki nchini Kenya inayopiga marufuku na au kuainisha misemo ya 'Hatupangwingwi' na 'Watajua Hawajui' kama matamshi ya chuki,” jaji Ndung’u alisema.

Mnamo mwezi Aprili, mwenyekiti wa tume ya NCIC Samwel Kobia alitoa orodha ya baadhi ya maneno ambayo tume hiyo iliyataja kuwa ya kuchochea umma na hivyo kuyapiga marufuku dhidi ya kutumika na wanasiasa humu nchini. Maneno hayo yalijumuisha ya lugha ya Kalenjin, Kiswahili na lugha ya mtaani almaarufu Sheng.