Raila apongeza Karua kuhusu mdahalo wa mgombea mwenza

"Familia ya Azimio inajivunia utendaji wako," Raila alisema.

Muhtasari

•Karua alichuana na naibu mgombea urais wa Kenya Kwanza Rigathi Gachagua katika sehemu ya pili ya mdahalo wa urais uliochukua dakika 90.

Mgombea urais wa Azimio la Umoja Raila Odinga na mgombea mwenza Martha Karua wakutana wakati wa uzinduzi wa manifesto ya muungano huo.
Mgombea urais wa Azimio la Umoja Raila Odinga na mgombea mwenza Martha Karua wakutana wakati wa uzinduzi wa manifesto ya muungano huo.
Image: STAR

Mgombea urais wa Azimio Raila Odinga amesema kuwa anajivunia utendakazi wa mgombea mwenza Martha Karua katika mdahalo wa urais.

Akizungumza Jumatano, Raila alimsifu waziri huyo wa zamani wa Sheria kwa umwerevu wake wa masuala yaliyoibuliwa katika mjadala na utulivu.

 

Aliongeza kuwa familia ya Azimio ilifurahishwa na utendaji wake.

"Utulivu wako, umahiri wako wa masuala ya somo, na kuwa mtulivu hata ulipochokozwa kulivutia. Nampongeza naibu wangu hodari na mwanachama wa timu Martha Karua. Familia ya Azimio inajivunia utendakazi wako wakati wa mjadala wa jana usiku. Endelea kuuza," Raila alisema kwa ukurasa wake wa tweet.

Karua alichuana na naibu mgombea urais wa Kenya Kwanza Rigathi Gachagua katika sehemu ya pili ya mdahalo wa urais uliochukua dakika 90.

Sehemu ya kwanza ya mdahalo huo ilihusisha mgombea mwenza wa Roots Party Justina Wamae na Ruth Mutua wa Agano Party.

Katika mjadala huo, Karua alidhibitisha kukuwa na  imani katika rekodi ya kinara wake Raila Odinga, akisema kuwa pamoja na rekodi yake, wana nafasi nzuri zaidi ya kupeleka nchi mbele.

"Nitakuwa naibu wa rais ambaye anaheshimu Katiba, watu wa Kenya, wa mkuu wangu na mtu ambaye atatii sheria, na kufanya kila linalowezekana kumuunga mkono nahodha wangu kufanikisha nchi hii," alisema.

Alibainisha kuwa kesi kama vile naibu wa rais kutokubaliana na Rais hadharani hazitaonekana hadharani kama ilivyokuwa kwa serikali ya Jubilee.

Karua alibainisha kuwa kila mara watasuluhisha tofauti zao bila ya watu wengine kujua, si jinsi ilivyokuwa  kati ya Rais Uhuru Kenyatta na William Ruto, na kwamba atamruhusu Raila kuongoza nchi.