Raila: Eti sitaongoza juu sijatahiriwa, walijuaje kama si mashoga? Mimi najua Luo, Teso, Turkana hatutahiri!

Raila aliwasuta wale wanaosema kwamba mtu hajatahiriwa hawezi kuwa rais wa nchi ya Kenya.

Muhtasari

• “Ile kitu mimi najua ni kwamba Waturkana, Wajaluo na Wateso hawatahiri" - Raila Odinga.

KInara wa ODM Raila Odinga
Image: George Owiti

Mpeperusha bendera wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga kwa mara nyingine tena amewasuta wale wapinzani wake wanaojipigia debe kwa kusema kwamba Raila hawezi kuongoza taifa la Kenya kwa tuhuma eti bado hajatahiriwa.

Akizungumza katika eneo la Morulem kwenye kaunti ya Turkana Jumatano katika moja ya msururu wa kampeni zake kaskazini mwa nchi, Raila alisema kwamab siasa kama hizo zimepitwa na wakati na ni wakati watu kuuza sera zao pasi na kuwakosea wenzao heshima.

Aidha, kinara huyo mkongwe kwenye fani ya siasa za Kenya alisema kwamab hao wote wanaosema hajatahiriwa aliwahi waliuliza walijuaje hajatahiriwa na ni wanaume wenzake.

“Kuna wale wanakuja na porojo nyingi zaidi, wakikaa kule wanasema eti ooh Raila hawezi kuongoza maanake yeye hajatahiriwa, hajatahiri. Nilimuuliza yeye, unajuaje Raila hajatahiri na wewe ni mwanaume kama Raila. Una haja gani na chombo cha mwanaume mwenzako?” alisema kinara huyo wa chama cha ODM.

Raila alisema kwamba wanaume wote hao ambao wanazua mijadala kuhusu mwanaume mwenzao kutahiri au kutotahiri bila shaka ni shoga.

Vile vile mwaansiasa huyo alionekana kukubaliana na madai hayo kwa kile alisema kwamba kitu yeye anajua kuna baadhi ya jamii humu nchini ambao hawatahiri na ni sehemu ya tamaduni na mila zao.

“Ile kitu mimi najua ni kwamba Waturkana, Wajaluo na Wateso hawatahiri. Sasa yeye anasema ati wewe na mjukuu wako na hata vitukuu wako hawawezi kuongoza maanake hamjatahiri, hiyo ni haki kweli? Si huo ni ujinga? Si huyo ni mpumbavu?” Raila aliuliza umati.

Kwa muda mrefu viongozi wanaoegemea mrengo wa Kenya Kwanza unaoongozwa na William Ruto wakiwemo Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria wamekuwa wakimshambulia Raila pamoja na jamii yake kwamba kwa kuwa hawatahiri basi hawana hadhi yoyote ya kuwa viongozi wa nchi.

Miezi michache iliyopitqa mbunge huyo ambaye ni mtetezi mkubwa wa sera za naibu rais William Ruto alizua mjadala mitandaoni alipodai kwamba Raila hajatahiriwa na waliambiwa na wazee wao kwamba kamwe uongozi hauwezi kuenda kwa mikono ya mtu ambaye hajapitia mila hiyo ya kisu.