(Video) Junet: Raila hatoshiriki mdahalo wa urais, tutatuma Babu Owino apambane na Ruto

Kulingana na Junet, Ruto si kiwango cha Raila na badala yake Babu Owino ndiye kiwango chake.

Muhtasari

• Mbunge huyo alisema kwamba iwapo masuala ya uongozi, uadilifu na ufisadi hayatozungumziwa basi Raila hatoshiriki.

Siku moja baada ya mpeperusha bendera wa vuguvugu la Kenya Kwanza William Ruto kutoa hakikisho kwamba atahudhuria mdahalo wa wagombea urais Jumanne wiki kesho, sasa madai yameibuka kutoka kwa mrengo pinzani wa Azimio la Umoja One Kenya wakisema kwamba huenda mpeperusha bendera wao hatoshiriki mdahalo huo.

Katika moja ya msafara wa kampeni zao huko Kitale kaunti ya Trans Nzoia, baadhi ya viongozi wa muungano huo walidokeza kwamab huenda Raila atasusia mdahalo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na idadi nyingi ya Wakenya.

Mbunge wa Suna ya mashariki, Junet Mohammed ambaye ni mkosoaji mkali wa naibu rais William Ruto alikashfu mdahalo huo na kusema kwamba ni aibu kumuweka Raila kwenye meza Moja na Ruto katika mdahalo.

“Baba atakuwa kwenye mdahalo ule, na hayo ni maoni yangu si maoni yake, atakuwa kwa mdahalo kama watazungumzia masuala matatu. Kama watazungumzia mambo ya uadilifu, ufisadi na uongozi. Kama kuna mambo mengine basi sisi kama Azimio la Umoja One Kenya tutamtuma mheshimiwa Babu Owino kushiriki kwa niaba ya Baba ili apambane na William Ruto,” Junet alisema kwa kejeli.

Maneno haya yanakuja siku chache tu baada ya mkurugenzi wa mawasiliano katika kamati ya kampeni za Raila, Dennis Onyango kudokeza kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba Wakenya wasikuwe na matumaini makubwa sana ya Raila kushiriki mdahalo, kwa kile alikitaja kuwa mdahalo wa wagombea wenza haukuwa na mihemko na ladha iliyotarajiwa na Wakenya wengi.

Mdahalo wa wagombea urais unazidi kukumbwa na misukosuko kadha baada ya Ruto jana kutoa sharti kwamba hata kama amekubali kushiriki lakini pia alitaka kufahamu kila suala litapewa muda wa dakika ngapi kuzungumziwa.

Isitoshe, mgombea urais kutoka chama cha Roots, wakili msomi George Wajackoyah naye Ijumaa asubuhi alitishia kususia mdahalo huo kwa kusema kwamab hawezi shiriki kama hawatakuwa na wagombea wengine watatu kwenye meza moja.

Ratiba ya midahalo hiyo imekuwa ikibagua wagombea kulingana na vigezo mbalimbali, kikubwa kikiwa ni kulingana na ufuasi ambao mgombea ako nao.