"Msiache ng'ombe afe na maziwa, badilisha 'aila' na 'uto' kwa herufi R" - Neslson Havi

Nelson Havi alionekana kwenye video akiwa na kofia zenye nembo ya Raila na kuwafanya wengi waamini amebadilisha msimamo wa kisiasa.

Muhtasari

• "Ni ghali mno kutengeneza kofia, kwa hiyo tunachukua za Azimio na kuzibadilisha" - Havi

Wakili na mwanasiasa Nelson Havi
Wakili na mwanasiasa Nelson Havi
Image: Facebook//NelsonHavi

Wakili msomi ambaye pia analenga kiti cha ubunge cha Westlands kupitia chama cha UDA, Nelson Havi amezua utata kwa mara nyingine tena baada ya kuonekana kwenye kofia iliyokuwa imeandikwa jina la kinara wa UDA William Ruto huku herufi R ikiwa ni nembo ya mpeperusha bendera mshindani wa Ruto, Raila Odinga.

“Ni dili ambayo imeisha hii,” Havi aliandika kwenye Facebook yake ambako alipakia picha hizo.

Watu mbali mbali walibaki vinywa wazi wasijue la kusema baada ya Havi kupakia picha hizo. Baadhi walisema ni ubunifu wa hali ya juu huku wakimpigia debe kwamab hivyo ndivyo atakavyoimarisha ubunifu miongoni mwa watu wa Westlands pindi atakaposhinda kama mbunge katika uchaguzi mkuu wa mapema mwezi kesho.

Kulingana na Havi, herufi hiyo ya R inawakilisha Ruto na wala si Raila kama ambavyo wengi wamekuwa wakijua kutokana na kutumiwa kama nembo ya Raila katika vifaa vya kampeni vya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya

Aliyekuwa mwanaharakati wa chama cha Jubilee kwa jina Polycarp Hinga alijaribu kujua Havi anamaanisha nini kwa kuonekana kaka vuguvugu sana watu wasimjue kama yupo upande wa Ruto ama upande wa Raila ambapo Havi alimjibu kwamba Ng’ombe hafai kufa na maziwa.

“Wakili usiogope Farouk hivo, kama roho iko kwa Baba, iko kwa Baba,” Hinga aliandika.

“Hujambo Polycarp, katika lugha ya Kalenjin tunasema ‘Ngombe asiruhusiwe kufa na maziwa’ Ni ghali mno kutengeneza kofia, kwa hiyo tunachukua za Azimio na kuzibadilisha zinakuwa zetu,” Havi alijibu kwa ujanja mithili ya sungura.

Kulingana na Havi, Raila ni kama ng’ombe anayeelekea kichinjioni na aliwataka wakenya haswa vijana kutomzika ng’ombe huyo akiwa na maziwa yake kwa maana ya kofia. Aliwataka kuchukua kofia na vitu vingine vyenye nembo ya Raila na kuondoa ‘aila’ katika jina lake na badaal yake kubadilisha herufi hizo na ‘uto’ kuunda Ruto.

“Wanaume na wanawake kati ya miaka 19 na 35, nyinyi ni wapiga kura waliojiandikisha milioni 8.8 kwa idadi na 39% ya wapiga kura wote. Tumia haki yako ya kupiga kura kwa busara. Mpigie kura Dkt William Ruto kuwa Rais na Nelson Havi mbunge, Westlands. Ongeza tu 'uto' kwa 'R'. Usizike ng'ombe na maziwa yake,” Havi aliandika.

Havi analenga kuwa mbunge wa Westlands kupitia UDA ambapo anataka kumg’atua mamlakani mbunge wa sasa wa ODM Tim Wanyonyi.