"Nitakusubiri" Ruto amsihi Raila kuhudhuria Mdahalo wa Urais

Ruto amefutilia mbali mikutano yote iliyopangwa kufanyika Jumanne.

Muhtasari

•Ruto amefutilia mbali mikutano yote iliyopangwa kufanyika Jumanne ili kumpa muda wa kutosha kujiandaa kwa mjadala ya urais.

•Ruto alisema ikiwa Raila hana ajenda ya kuwaambia wapiga kura, angalau awaeleze maana ya misemo anayotumia wakati wa kampeni.

wakati wa kampeni huko Nandi Hills, Kaunti ya Nandi mnamo Jumatatu, Julai 25,2022.
Naibu Naibu Rais William Ruto wakati wa kampeni huko Nandi Hills, Kaunti ya Nandi mnamo Jumatatu, Julai 25,2022.
Image: FACEBOOK// WILLIAM RUTO

Mgombea urais wa Kenya Kwanza William Ruto amefutilia mbali mikutano yote iliyopangwa kufanyika Jumanne.

Haya ni kulingana na tangazo la mtaalamu wa mikakati wa kidijitali wa UDA Dennis Itumbi.

Hatua wii ni ili kumpa muda wa kutosha kujiandaa kwa mjadala ya urais utakaofanyika katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (CUEA).

"Ruto ataghairi mikutano yote iliyoratibiwa kufanyika Kesho, Jumanne, Julai 26, 2022. Ili kumwezesha kujiandaa kwa Mjadala wa Urais," Itumbi alisema Jumatatu kupitia Facebook.

Kiongozi huyo wa UDA alitarajiwa kuuza ajenda zake kwa wakazi wa kaunti za Baringo, Nakuru na Nyandarua.

Akizungumza wakati wa kampeni katika kaunti za Uasin Gishu na Nandi mnamo Jumatatu, Ruto pia alimsihi mpinzani wake wa Azimio Raila Odinga kujitokeza kwa mdahalo huo.

“Nataka kumtia moyo mshindani wangu, Bw Kitendawili, kufikiria upya kuja kwenye mdahalo, nitakusubiri,” alisema.

Ruto alisema ikiwa Raila hana ajenda ya kuwaambia wapiga kura, angalau awaeleze maana ya misemo anayotumia wakati wa kampeni.

"Hata kama huna sera au mipango yoyote, tafadhali njoo kwenye mjadala kwa sababu Wakenya wanataka kujua hii 'tibim' na 'tialala' ni nini. Wanataka kujua hizi ngano zenu zina maana gani."

Matamshi yake yanajiri baada ya msemaji wa Azimio Makau Mutua Jumapili kudokeza kuwa huenda Waziri Mkuu huyo wa zamani hatahudhuria mjadala huo.

Alidai DP alipanga kuhakikisha kuwa hakuna mijadala kuhusu ufisadi na uadilifu, na kuongeza kuwa hayo ndiyo masuala ya msingi katika ajenda ya Muungano.

Mutua alisema Ruto hajali maadili, miongozo ya umma wala aibu.

"Ndiyo maana hatuna nia ya kushiriki jukwaa la kitaifa na mtu ambaye hana adabu. Kama inavyojulikana, mpinzani wetu alizunguka nchi akitutupia maneno ya kashfa pamoja na viongozi wengine wakuu wa kitaifa, ikiwa ni pamoja na mashambulizi mabaya ya kingono," alisema.