Ruto ajibu madai ya kuwa na 'pupa' ya ardhi

Ruto alisisitiza kuwa ardhi yote anayomiliki ilichukuliwa kihalali.

Muhtasari

•Akizungumza wakati wa mjadala wa Urais, Ruto alisisitiza kuwa ardhi yote anayomiliki ilichukuliwa kihalali.

•Alisema kuwa watu waliomlaghai kuhusu ardhi ya Muteshi kwa sasa wapo mahakamani kuhusu na kesi inaendelea.

akizungumza katika mdahalo wa urais uliofanyika CUEA mnamo Julai 26, 2022
Naibu rais William Ruto akizungumza katika mdahalo wa urais uliofanyika CUEA mnamo Julai 26, 2022
Image: PRESIDENTIAL DEBATE SECRETARIAT

Mgombea urais wa Kenya Kwanza William Ruto amesema kuwa hana hamu ya ardhi.

Akizungumza wakati wa mjadala wa Urais, Ruto alisisitiza kuwa ardhi yote anayomiliki ilichukuliwa kihalali.

Aliendelea kusema kuwa yeye pia alikuwa mhanga wa wauzaji ardhi walaghai kuhusiana na sakata ya ardhi ya Muteshi.

Ruto alisema kuwa mahakama ilimuamuru amlipe mmiliki wa shamba hilo kwa muda wote aliokuwa 'akimilimiki.'

"Kipande chochote cha ardhi nilichonacho kilichukuliwa kihalali. Nilikuwa mhasiriwa wa ardhi ya ulaghai. Mahakama iliniamuru kufanya ni kulipa kwa miaka mitatu niliyokuwa kwenye ardhi hiyo," alisema.

Aliongeza kuwa watu waliomlaghai kwa sasa wapo mahakamani kuhusu ardhi hiyo na kesi inaendelea.

Adrian Muteshi alifukuzwa kutoka Eldoret wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 na shamba lake kuchukuliwa.

Alimshutumu Ruto kwa kuchukua shamba lake la ekari 100 huko Uasin Gishu kinyume cha sheria na kuomba mahakama kuingilia kati.

Mahakama Kuu jijini Nairobi iliamuru kwamba Muteshi alithibitisha kuwa mali hiyo ni yake na kwamba alikuwa amenyang'anywa.

Kwa upande wake, Ruto aliagizwa kulipa Sh5 milioni kwa mwathiriwa huyo wa ghasia za baada ya uchaguzi kwa kunyakua ardhi yake kinyume cha sheria.

Ruto kupitia kwa mawakili wake alisema kuwa yeye ni mnunuzi asiye na mashaka ambaye alisikia kuwa kuna ardhi ilikuwa ikiuzwa na kufanya uangalizi kabla ya kuinunua kutoka kwa watu alioamini kuwa ndio wamiliki wa mali hiyo.

Muteshi, 86, alifariki jijini Nairobi Oktoba 2020.