Sababu za Raila kususia Mdahalo wa Urais- Ruto

Ruto alimshtumu kiongozi huyo wa ODM kwa kuogopa kujibu maswali magumu.

Muhtasari

•DP pia alimshtumu kiongozi huyo wa ODM kwa kuogopa kujibu maswali magumu ilhali amekuwa kwenye serikali.

•Naibu rais  pia alidai kuwa kutokuwepo kwa Raila kwenye mdahalo huo wa kitaifa ni dharau kwa Wakenya

akizungumza wakati wa mdahalo wa urais uliofanyika CUEA mnamo Julai 26, 2022
Naibu Rais William Ruto akizungumza wakati wa mdahalo wa urais uliofanyika CUEA mnamo Julai 26, 2022
Image: EZEKIEL AMINGA

Mgombea urais wa Kenya Kwanza Dkt William Ruto amedai kuwa mwenzake wa Azimio-One Kenya Raila Odinga alisusia mdahalo wa urais uliofanyika  Jumanne usiku kwa kuwa hana ajenda za kuwauzia Wakenya.

Ruto alijipata akijadili pekee yake baada ya aliyekusudiwa kuwa mshindani wake katika mdahalo, Raila Odinga kukosa kufika katika Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afrika Mashariki ambako mdahalo ulifanyika.

Akizungumza wakati wa mdahalo, naibu rais alidai kuwa yeye ndiye mgombea urais pekee aliye na mpango kwa Wakenya.

"Mshindani wangu hayupo hapa kwa sababu hana mpango. Hana ajenda. Hawezi kueleza lolote kwa watu wa Kenya," Ruto alisema.

DP pia alimshtumu kiongozi huyo wa ODM kwa kuogopa kujibu maswali magumu ilhali amekuwa sehemu ya serikali katika muhula wa pili wa utawala wa rais Kenyatta.

"Kusema kweli, mshindani wangu hata hangekuja hapa kwa sababu yeye siye mgombea halisi, yeye ni mradi. Mengine ni vijisababu tu. Anaepuka maswali magumu, hataki kujibu," Alisema.

Raila alikosa kuhudhuria mdahalo huo ambao uling'oa nanga saa mbili usiku hadi mwendo wa saa tatu unusu kama alivyokuwa amedokeza hapo awali.

Siku chache zilizopita msemaji wa Azimio Makau Mutua alidokeza kuwa Waziri Mkuu huyo wa zamani hangehudhuria mdahalo huo.

Mutua alidai DP alipanga kuhakikisha kuwa hakuna mijadala kuhusu ufisadi na uadilifu, huku akiongeza kuwa hayo ndiyo masuala ya msingi katika ajenda ya Azimio. Pia alisema kuwa Ruto hajali maadili, miongozo ya umma wala aibu.

"Ndiyo maana hatuna nia ya kushiriki jukwaa la kitaifa na mtu ambaye hana adabu. Kama inavyojulikana, mpinzani wetu alizunguka nchi akitutupia maneno ya kashfa pamoja na viongozi wengine wakuu wa kitaifa, ikiwa ni pamoja na mashambulizi mabaya ya kijinsia," alisema kupitia taarifa.

Akizungumza baada ya kuhudhuria mdahalo huo, naibu rais alidokeza kuwa hakuridhika kufuatia kutokuwepo kwa mshindani wake.

"Natamani mshindani wangu angekuwepo ili Wakenya waweze kuangalia pande zote mbili. Kwa bahati mbaya lakini inayoeleweka, kuna mpango mmoja tu katika uchaguzi huu, wengine wako na mifano tu ndio maana hawapo hapa," Alisema.

Naibu rais  pia alidai kuwa kutokuwepo kwa Raila kwenye mdahalo huo wa kitaifa ni dharau kwa Wakenya