(Video) Babu Owino azuiliwa kuingia CUEA kumenyana na Ruto katika mdahalo wa urais

Mbunge huyo alisema kwamba alitumwa kuwakilisha Raila katika mdahalo huo lakini akazuiliwa.

Muhtasari

• “Niulikuja hapa hasa kujadili na Ruto katika masuala yenye umuhimu wa kitaifa, hata kama wameninyima kuingia" - Babu Owino.

Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino ameibua madai kwamab Jumanne alielekea katika chuo kikuu cha Kikatoliki ambako mdahalo wa urais ulikuwa unafanyika na akazuiwa kuingia ukumbinini ili kushiriki katika mdahalo huo na naibu wa rais William Ruto.

Babu Owino alisema kwamba alienda pale kumwakilisha mpeperusha bendera wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga ambaye alisusia kwa kusema kwamba hakutaka kukutana na Ruto uso kwa uso bali anataka wakutane debeni wiki mbili zijazo.

Katika video ambayo mbunge huyo alipakia kweney ukurasa wake wa Facebook ambayo aliichukua mbashara akiwa katika lango kuu la chuo hicho, anaonekana akizuiliwa kuingia na maafisa wa polisi.

“Kama mnavyoona, niko hapa katika lango la CUEA, na nimezuiwa kuingia na polisi ambao wanasema sifai kuingia hapa. Nilikuja hapa leo kumwakilisha Baba Raila Amollo Odinga kwa sababu niliteuliwa na kamati ya kampeni za Azimio kuwakilisha Raila katika mdahalo huu. Na pia niliteuliwa kuwakilisha maslahi ya Wakenya,” Babu Owino anaonekana akizungumza.

Wiki jana mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed alidokeza kwamba mpeperusah bendera wao Raila Odinga hangeshiriki mdahalo wa urais na badala yake wangemtuma mbunge Babu Owino kuwakilisha, kitu ambacho Owino alisema kwamba amekubali na jana alijitokeza kutimiza hilo kwani alikuwa na uchu wa kumenyana na mpeperusha bendera wa muungano wa Kenya Kwanza, William Ruto ambaye alikuwa tayari ashatua ukumbini tayari kwa mdahalo.

PREPARING for the DEBATE.I will deal with Ruto ORTHOGONALLY.

Posted by Babu Owino on Sunday, July 24, 2022

Owino alisema kwenye video hiyo kwamab angekubaliwa kuingia basi angeuliza maswali yenye ukakasi mkubwa kama kutaka kujua nini kilitendeka kwa afisa wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, Chris Musando pamoja pia na kutaka kudadisi kilichotokea kwa kesi iliyokuwa ikimkabili Ruto na rais Kenyatta katika mahakama ya kimataifa ya jinai, ICC huko Hague, Uholanzi.

“Niulikuja hapa hasa kujadili na Ruto katika masuala yenye umuhimu wa kitaifa, hata kama wameninyima kuingia, nilitaka kumdhalilisha Ruto katika mdahalo huu, hawa polisi naona wananichelewesha sana,” Babu Owino anaonekana akizungumza.