Raila amshauri Ruto kutafuta mgombea mwenza mwingine, asema Gachagua ana hatia ya ulaji rushwa

Raila alikuwa akizungumzia uamuzi wa mahakama kutwaa shilingi milioni 200 za Gachagua

Muhtasari

• Raila alisema kulingana na sheria kuhusu uadilifu Gachagua hafai kushikilia wadhifa wowote wa utumishi wa umma. 

KInara wa ODM Raila Odinga
Image: George Owiti

Mgombea wa Urais wa muungano wa Azimio la umoja One- Kenya Raila Odinga amesema kuwa mpizani wake wa Kenya Kwanza William Ruto hana mgombea mwenza katika kinya’nga’ nyiro cha Agosti 9. 

Raila alisema haya akiwa katika kampeni ya kusaka kura katika kaunti ya Machakos siku ya Ijumaa ambapo alikuwa akinadi sera zake huku akimkashifu vikali mpinzani wake wa Kenya Kwanza William Ruto. 

Bwana Odinga alikuwa akirejelea kesi ya ufisadi inayomwandama mbunge wa Maathira,Rigathi Gachagua ambaye ni mgombea mwenza wa  kiti cha urais wake Ruto. Awali, katika mdahalo wa wagombea wenza wa kiti cha Urais, Gachagua alikanusha madai kwamba pesa zake alizipata kwa njia ya ufisadi. 

Kufuatia uamuzi uliyotolewa na jaji Esther Maina, Serikali inafaa kuchukua  shilingi milioni 200 za Gachagua ambazo zilikuwa zimezuiliwa katika benki moja humu nchini kutokana na madai ya ufisadi. 

“Ruto hana mgombea mwenza maana anakabiliwa na kesi ya ufisadi. Si mlisikia jana kesi ilisema hizo pesa ni za uwizi,” Raila alisema. 

Akirejelea kipengele cha 6 cha katiba, kuhusu utendakazi na uadilifu wa maafisa wa umma, yeyote aliyehusishwa katika sakata au utovu wa maadili hafai kugombea kiti chochote au kushikilia wadhifa wa utumishi wa umma. 

Raila amesema kulingana na uamuzi wa mahakama, Gachagua hafai kuwa mgombea mwenza wa Ruto. 

“Kipengele cha sita cha katiba yetu hakiruhusu mtu yeyote aliyepatikana na hatia ya ufisadi kugombea kiti chochote,” Odinga alisema.