"Mimi ni mtoto wa mwisho wa Raila" Mwanariadha Ezekiel Kemboi ampigia debe Raila

Kemboi pia alinadi sera za Raila katika chaguzi za 2013 na 2017.

Muhtasari

• Kemboi alisema kwamba Raila ndiye atakayeshughulikia masuala ya vijana pasi na kupiga simu mara kwa mara.

Kinara wa ODM Raila Odinga
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Kadri muda unazidi kuyoyoma kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, miungano mbalimbali inazidi kurindima ngoma zao kujinadi na kujipigia debe katika sehemu mbalimbali za nchi kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa Wakenya wapiga kura.

Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya wikendi iliyopita walikita kambi katika bonde la ufa, eneo linalosemekana kuwa ni ngome ya mpeperusha bendera wa muungano wa Kenya Kwanza, William Ruto.

Katika hafla moja mjini Eldoret, palitokea jambo lisilo la kawaida ambapo aliyekuwa bingwa wa dunia katika mita elfu tatu kuruka viunzi Ezekiel Kemboi alipopewa nafasi ya kuzungumza alimpigia upato Raila Odinga kumshinda William Ruto katika kinyang’anyiro cha urais licha ya eneo hilo kutambulika kuwa wakaazi wake wengi ni wafuasi wa Ruto.

Kemboi alisema kwamba yeye anampigia upato mkubwa bwana Raila Odinga na hata kusema kwamba yeye ni mtoto wake wa mwisho.

“Nimekuja hapa kama mzaliwa wa mwisho wa Baba. Jina langu ni Ezekiel Kemboi Amollo. Na ukiniona hapa, uwe na uhakika kwamba mambo ya vijana yatatatuliwa na hakutakuwa na haja ya kupiga simu tena,” Ezekiel Kemboi alisema huku umati ukimshangilia kweli kweli.

Hii si mara ya kwanza kwa Kemboi kuonekana hadharani akimpigia debe Raila Odinga kwani katika chaguzi za mwaka 2013 na 2017, mwanariadha huyo alikuwa katika mstari wa mbele kuzinadi sera za Raila kipindi hicho akigombea kutoka kwa mirengo ya CORD na NASA mtawalia.