Bahati kama ya Igathe:Kazi 10 ambazo Igathe alipata bila kutuma maombi ya kutafuta kazi

Igathe alipata kazi yake ya kwanza pindi tu alipohitimu elimu ya chuo kikuu.

Muhtasari

• Igathe alijitosa kwenye siasa kwa mara ya kwanza mwaka 2017 alipopochaguliwa kama naibu gavana Nairobi na kuachia wadhifa huo miezi sita tu ofisini.

Mgombea ugavana kaunti ya Nairobi, Polycvarp Igathe
Mgombea ugavana kaunti ya Nairobi, Polycvarp Igathe
Image: Facebook//Polycarp Igathe Kamau

Nchini Kenya, utawasikia watu wanabananga msemo wa bahati kama ya mtende na kusema bahati kama ya Igathe, wengine utawasikia wanasema Mungu wa Igathe. Hivi huyu Igathe ni nani?

Polycarp Igathe ni jamaa msomi ambaye jina lake lilijinafasi katika ndimi za wengi baada ya ujio wake katika fani ya siasa za humu nchini. Wengi wamekuwa wakimhusisha na bahati kutokana na dhana kwamba Igathe tangu maisha yake ya ujana mpaka sasa anaelekea hamsini, amekuwa ni mtu wa kutafutwa na kazi, na si yeye kutafuta kazi kama ilivyo kawaida kwa watu wengi.

Katika Makala haya, tumekuandalia baadhi ya kazi ambazo mwanasiasa huyu amezifanya, kutoka maisha yake ya kazi za ukurugenzi kwenye maofisi mbalimbali ulimwenguni, hadi kwenye nyadhifa za kisiasa.

POLYCARP IGATHE KAMAU
POLYCARP IGATHE KAMAU

1. Afisa wa Kifedha - Queensland Health, Australia

Inasemekana kazi yake ya kwanza kabisa aliipata pindi tu alipohitimu chuo kikuu mwaka wa 1995 ambapo kampuni ya kimataifa ya afya kwa jina Queensland Health iliziwinda huduma zake kama afisa wa kifedha. Igathe aliifanya kazi hiyo kwa uadilifu kwa miezi kumi na minane tu ambapo alishiba na kuachia kabla ya kurudi nchini Kenya.

2. Mkufunzi wa usimamizi - CocaCola Africa

Kufika nchini Kenya hakukawia kwani kazi nyingine ilikuwa inamsubiria katika kampuni ya vinywaji ya Coca Cola Afrika ambapo aliingia kule kama mkufunzi wa usimamizi kwenye kampuni hiyo ambapo alizichabanga hadi mwaka wa 2000 kabla ya kugura tena.

3. Meneja wa mauzo na masoko - Africa Online

Polycarp Igathe hakuhangaika hata kidogo kutafuta kazi baada ya hapo kwani muda mchache baadae milango ya kampuni ya Africa Online, moja ya kampuni kubwa za huduma za mitandaoni kipindi hicho. Igathe alifanya kazi hapo kama meneja wa mauzo na masoko japo haijulikani ni kwa muda upi alidumu

4. Meneja wa uendeshaji wa mauzo - East Africa Breweries

Baada ya kuondoka Africa Online, Igathe slijiweka sawa na kuteuliwa tena kama  meneja wa uendeshaji wa mauzo katika kampuni ya vileo ya East Africa Breweries.

POLYCARP IGATHE KAMAU
POLYCARP IGATHE KAMAU

5. Mkurugenzi mtendaji - Haco

Kama hiyo haitoshi, mnamo mwaka 2003 Igathe aliingia kwenye kampuni ya hayati Chris Kirubi, Haco kama mkurugenzi mtendaji ambapo alidumu kwa muda wa miaka 10. Baada ya kampuni hiyo kuuzwa kwa msimamizi mwingine, Igathe alibwaga manyanga ila tena hakukaa nje sana.

6. Mkurugenzi mtendaji - Vivo

Mwaka 2014, Igathe aliingia katika kampuni ya kawi ya Vivo kama mkurugenzi mtendaji wa kwanza kabisa kutoka Kenya, baada ya kampuni hiyo kuchukua umiliki wa kampuni ya kuuza petroli ya Shell katika mataifa 16 barani Afrika. Hapa alizipiga hadi mwaka wa 2017 kabla ya kujitosa kweney siasa.

POLYCARP IGATHE KAMAU
POLYCARP IGATHE KAMAU

7. Mwenyekiti - Chama cha Watengenezaji wa Kenya

Lakini kabla ya kujitosa kwenye siasa, Igathe alikuwa ametwikwa jukumu la mwenyekiti wa Chama cha Watengenezaji wa Kenya kati ya mwaka 2012-2014.

8. Mwenyekiti - Taasisi ya Petroli ya Afrika Mashariki

Pia alihudumu kama mwenyekiti wa Taasisi ya Petroli ya Afrika Mashariki kati ya mwaka 2014-2016 miongoni mwa majukumu mengine madogo madogo kama Mkurugenzi na Mdhamini wa Muungano wa Sekta ya Kibinafsi ya Kenya na mwenyekiti na mjumbe wa Bodi ya Usimamizi ya Shule ya Upili ya Wasichana ya Bishop Gatimu Ngandu tangu kati ya mwaka 2010 hadi 2017.

9. Naibu gavana - Nairobi

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017, Igathe alishikana mkono na mwanasiasa Mike Sonko katika kujaribu bahati yao kuchukua nafasi ya uongozi wa kaunti ya Nairobi, Sonko akiwa kama gavana na Igathe mgombea mwenza. Sonko na Igathe waliapishwa kama gavana na naibu wake baada ya kushinda kwa tikiti ya chama cha Jubilee. Lakini Igathe kwa mara nyingine tena hakudumu kwenye wadhifa huo kama kawaida yake kwani alijiuzulu baada ya miezi sita tu ofisini kama naibu gavana.

POLYCARP IGATHE KAMAU
POLYCARP IGATHE KAMAU
Image: POLYCARP IGATHE KAMAU

10. Afisa Mkuu wa kibiashara - Equity gropu holdings

Mnamo mwezi Mei mwaka 2018 tena bahati ikabisha mlangoni pake, safari hii kutoka kwa benki ya Equity ambayo ilizitaka huduma zake kuwa kama afisa mkuu wa kibiashara, nafasi ambayo Igathe aliiwakilisha kwa muda mchache kabla tena ya kurejea kwa mara ya pili kwenye kampuni ya kawi ya Vivo alikofanya kazi kwa miezi saba tu kabla ya kujiuzulu na kurudi Equity tena.

Jina lake liliibuka kwenye tasnia ya kisiasa tena mwezi Aprili mwaka huu ambapo chama cha Jubilee kilimpendekeza kuwa mgombea ugavana Nairobi kwa niaba ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya. Mgombea mwenza wake ni aliyekuwa mbunge wa Kibwezi, profesa Philip Kaloki.