Gachagua asimulia jinsi watu wasioujulikana walivyojaribu kuingia kwenye chumba chake

Gachagua aliibua madai kwamba kundi la wasiojulikana wamekuwa wakimfuata kwa muda.

Muhtasari

• Jumamosi mbunge huyo wa Mathira aliwashangaza Wakenya baada ya kusema maisha yake yamo hatarini.

• Gachagua alisema kwamba watu wasiojulikana walimfuata hadi kwenye chumba chake cha hoteli wakitaka kuingia.

Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua
Image: EUTYCAS MUCHIRI

Mgombea mwenza wa urais wa UDA Rigathi Gachagua amezua taharuki kwa madai mapya yanayohusu vitisho vya maisha yake.

Jumamosi mbunge huyo wa Mathira aliwashangaza Wakenya baada ya kusema maisha yake yamo hatarini.

 Aliibua  madai kwamba kundi la wasiojulikana wamekuwa wakimfuata kwa muda.

Katika mahojiano ya kipekee na Star, mbunge huyo wa muhula wa kwanza alifichua undani kuhusu vitisho dhidi ya maisha yake. 

"Nimekuwa nikinyanyaswa na serikali kwa miaka minne iliyopita. Tangu niwe mgombea mwenza, serikali imeongeza ufuatiliaji juu yangu na familia yangu," alisema.

 Siku moja baada ya kulalamika hadharani, Gachagua aliambia gazeti la Star kwamba watu wasiojulikana walimfuata hadi kwenye chumba chake cha hoteli wakitaka kuingia.

 "Nilipolala Nakuru siku ya Ijumaa, kulikuwa na watu wasiojulikana waliokuwa wakiniulizia. Walikuja kabla sijaingia chumbani mwangu ambapo walitaka kuingia lakini wakazuiliwa," alisema. 

"Na usiku, nilisikia watu wakizunguka kwenye korido. Nilipotoka, walitoweka." 

Mgombea mwenza wa DP William Ruto hakuweza kufichua maelezo ya hoteli aliyolala na kwa hivyo Star haikuweza kufuatilia maswali muhimu kama vile picha zozote za CCTV ndani ya kituo hicho ili kutambua sura za watu hao.

Gachagua pia hakuweza kueleza jinsi hoteli ile ile iliyowanyima watu kuingia kwenye chumba hicho inaweza kuruhusu kundi hilo kutembea kwenye korido.

Mara baada ya IEBC kutangaza kwenye gazeti la serikali majina ya wagombea Urais na Naibu wa urais, Inspekta Jenerali wa polisi anahitajika kuwapa, maafisa wa usalama waliojihami. 

Maafisa hao wametumwa nyumbani kwao, jijini na vijijini. Angalau maafisa wawili watahitajika kutoa usalama kwa msingi wa saa 24. 

Kikosi cha maafisa watano kitahitajika kuandamana nao katika kampeni zao ili kuhakikisha ulinzi wa hali ya juu.  

Timu hiyo inaongozwa na afisa wa cheo cha mkaguzi ambaye anatakiwa kuwasiliana kila mara na makamanda wa polisi wa sehemu yoyote watakayotembelea kwa sababu za kiusalama.

Wagombea hao pamoja na wagombea wenza wao wanatarajiwa kuwashughulikia maofisa waliokabidhiwa. 

Hii ni pamoja na kuwapa vyumba vya walinzi na magari ya kutumia kwa harakati zao. 

Ingawa Gachagua ana haki ya kupata usalama kama Naibu mgombeaji urais, nyumbani kwake na akiwa kwenye kampeni, mbunge huyo alisema hajui jinsi wanavyofanya kazi.

 “Serikali imenipa wanausalama kadhaa, siwajui,  sijui wameambiwa nini, wapo. namuamini Mungu tu wapo sawa na wana nia njema, nina wasiwasi,” alisema.

Gachagua ni mmoja wa Washirika watatu wa Ruto waliodai kuwa maisha yao yako hatarini. 

Madai hayo yanafuatia mkutano wa Rais Uhuru Kenyatta uliofanyika Nakuru Alhamisi ambapo alidaiwa kusema Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, mwenzake wa Kiharu Ndindi Nyoro, Rigathi na Ruto watajua yeye ndiye rais. 

Matamshi hayo yalizua vita vya maneno huku Ruto akiongoza timu yake katika mashambulizi ya kivita dhidi ya Rais.

Akiwa katika kampeni katika Kaunti ya Nandi mnamo Ijumaa, Ruto alimkashifu bosi wake kwa madai ya vitisho. 

"Sisi ndio tuliokupigia kura, na sasa unataka kunitishia? Bora tu usiue watoto wangu tuheshimiane," alisema. 

Uhuru, hata hivyo, mnamo Jumapili alikanusha madai ya njama za kumwangamiza mtu yeyote. 

Rais alisema amekuwa akikabiliwa na dhuluma na mashambulizi kutoka kwa DP Ruto kwa miaka minne iliyopita lakini hakuna aliyedhulumiwa. 

“Hakuna haja ya kuwaambia watu kwamba nataka kukuua. Hujanitukana kwa miaka mitatu? Kuna mtu amekugusa?" Uhuru alihoji.