Fahamu wanasiasa wanaovalia jaketi za mikono mifupi kwenye kampeni

Ni kama njia mpya ya kujitia chapa na kujizolea umaarufu miongoni mwa wananchi wapiga kura.

Muhtasari

• Kwenye orodha hiyo, wanasiasa wengi kutoka mrengo wa Kenya Kwanza wameukumbatia mtindo huu wa fasheni.

William Ruto, Raila Odinga, Edwin Sifuna, Cleophas Malala
William Ruto, Raila Odinga, Edwin Sifuna, Cleophas Malala
Image: Twitter

Kenya inapojiandaa kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, kwa mara nyingine tena wanasiasa mbalimbali wakuu wamekuja na njia mpya za kujitia chapa kwa njia za kipekee ili kuwavutia wananchi ambao ndio wapiga kura.

Katika Makala haya, tumezamia wanasiasa ambao wamekumbatia fasheni ya kuvalia jaketi nzito zenye mikono mifupi ambazo wengi wao wamezitia chapa ya nembo zao na wengine hadi wakivalia jaketi hizo zenye rangi zinazoambatana na utambulisho wa vyama na miungano.

1. William Ruto – Mpeperusha bendera wa Kenya Kwanza

William Ruto ni naibu wa sasa wa Kenya ambaye analenga kujaribu bahati yake katika nyadhifa ya urais kwa mara ya kwanza kabisa kupitia chama chake cha UDA. Chama hicho kiko chini ya mwavuli wa Kenya Kwanza ambao utambulisho wake ni toroli na rangi mchanganyiko wa njano na kijani.

William Samoei Ruto
William Samoei Ruto

2. Rigathi Gachagua – Mgombea mwenza wa Ruto

Huyu ni mbunge wa sasa wa Mathira, eneo bunge linalopatikana kaunti ya Nyeri. Gachagua kwa kipindi kimoja aliwahi hudumu kamqa msaidizi wa rais Kenyatta kipindi hicho akiwa naibu Waziri mkuu. Ni mgombea mwenza wa William Ruto katika kinyang’anyiro cha urais.

Rigathi Gachagua
Rigathi Gachagua

3. Raila Odinga – Mpeperusha bendera wa Azimio

Raila Odinga
Raila Odinga

Ni mwanasiasa mkongwe ambaye anatambulika na wengi katika kuwa mstari wa mbele kupigania uhuru wa vyama vingi dhidi ya serikali dhalimu ya rais hayati Daniel Moi. Odinga kwa sasa ni mpeperusha bendera wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ambapo anajiongeza kama kinara wa chama cha ODM wa muda wote. Anawania urais kwa mara ya tano katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

4. Martha Karua – Mgombea mwenza wa Odinga

Mama mchapakazi ambaye ni wakili na mwanaharakati wa haki za kibinadamu ambaye ni kinara wa chama cha NARC Kenya. Martha Karua ni miongoni mwa wanawake wachache ambao wamedumu kwenye fani ya siasa za miongo mingi huku akitambulika na misimamo yake mikali ndidi ya serikali za marais wa awali Moi na Kibaki.

5. Musalia Mudavadi – Kinara wa ANC

Musalia Mudavadi
Musalia Mudavadi

Alijipata kwenye siasa kipindi cha serikali ya Moi wakati ambapo rais huyo alimteua kwenye baraza lake la mawaziri. Mudavadi aliwahi kuhudumu kama Waziri wa fedha miongoni mwa nyadhifa nyingine nyingi kabla ya kuwania urais mwaka wa 2013 na kumaliza wa tatu nyuma ya rais Kenyatta na Odinga. Kwa sasa, yeye ni mmoja wa vinara wa muungano wa Kenya Kwanza kumpigia debe Ruto kuelekea ikulu.

6. Moses Wetangula – Kinara wa FORD-K

Kinara wa chama cha FORD-K ambacho ni moja ya vyama tanzu ndani ya muungano wa Kenya Kwanza. Ni seneta wa sasa wa kaunti ya Bungoma.

Moses Wetangula
Moses Wetangula

7. Polycarp Igathe – Mgombea ugavana Nairobi

Huyu hana historia ndefu sana katika siasa ila alijulikana mnamo mwaka 2017 alipoteuliwa kama naibu gavana wa Nairobi, wadhifa ambao aliuachia miezi sita baadae. Analenga kuwa gavana Nairobi kupitia chama cha Jubilee.

Polycarp Igathe
Polycarp Igathe

8. Esther Passaris – Mwakilishi wa kike Nairobi

Analenga kutetea nyadhifa yake ya kuwa mwakilishi wa kike katika kaunti ya Nairobi kwa mara ya pili kupitia tikiti ya chama cha ODM. Aliteuliwa mara ya kwanza 2017 alipombwaga Rachel Shebesh ambaye alikuwa mwakilishi wa kwanza wa kike.

9. Edwini Sifuna – Katibu mkuu ODM

Mwanasiasa mchanga ambaye anashikilia nafasi ya katibu mkuu katika chama cha ODM. Kwa sasa analenga kuwa seneta wa Nairobi kupitia chama cha ODM.

10. Kimani Wamatangi – Seneta wa Kiambu

Ni seneta wa Kiambu aliyeteuliwa kwa chama cha Jubilee. Aliteuliwa kama kiranja wa walio wengi kwenye bunge la seneti baada ya seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata kunyang’anywa mamlaka hayo kwa kuonekana kuegemea mrengo wa Ruto. Wamatangi pia mapema mwaka huu alinyang’anywa mamlaka hayo kwa kujiunga na mrengo wa Ruto. Analenga kuwa gavana wa Kiambu kupitia chama cha UDA.

Kimani Wamatangi
Kimani Wamatangi