IEBC yapokea shehena ya mwisho ya karatasi za kupigia kura

Vituo vyote 46,229 vya kupigia kura vimechapishwa kwenye gazeti la serikali.

Muhtasari

• Katika tukio la hitilafu ya mtandao, Tume ilisema vifaa vya KIEMS vimewekwa sim kadi za GSM za msingi na za upili ili kuhakikisha uendelevu.

 

MWENYEKITI WA IEBC WAFULA CHEBUKATI
Image: EZEKIEL AMING'A

Shehena ya mwisho ya karatasi za kupigia kura inawasilishwa nchini Jumatano kabla ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Jumanne wiki ijayo.

IEBC iliongeza kuwa vituo vyote 46,229 vya kupigia kura nchini vimechapishwa kwenye gazeti la serikali.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema, vifaa vyote vya KIEMS viko tayari kusambazwa kwa maeneo mbali mbali huku kila wadi ikitengewa vifaa sita vya ziada vya KIEMS.

“Vifaa vyote vya KIEMS vimetayarishwa na tayari kutumwa kwa Wasimamizi wa Uchaguzi kabla ya kutumwa kwa maafisa wa uchaguzi na vifaa vingine vya uchaguzi. Vifaa vyote vya KIEMS vinaambana na kifaa cha kuhifadhi umeme ambacho kitajazwa umeme kabla ya kutumwa,” Chebukati alisema.

Katika tukio la hitilafu ya mtandao, Tume ilisema vifaa vya KIEMS vimewekwa sim kadi za GSM za msingi na za upili ili kuhakikisha uendelevu. Modemu za setilaiti zitatumwa kama hifadhi rudufu.

"Kwa madhumuni ya uwasilishaji wa matokeo kielektroniki, vifaa vya KIEMS vimewekwa sim kadi za msingi na za upili za GSM ili kuhakikisha uendelevu wa mtandao ikiwa moja itashindwa. Tume pia itatumia modemu za satelaiti kama nakala rudufu na ikiwa itashindwa, afisa Msimamizi atawasilisha matokeo kutoka kwa Kituo cha Kujumlisha Mahesabu ya Eneobunge mbele ya maajenti,” Chebukati aliongeza.

Iwapo kutakuwa na matukio ya dharura kama vile mafuriko ya ghafla, vurugu au ukosefu wa usalama, afisa msimamizi atawasilisha matokeo katika Kituo cha Kujumlisha Mahesabu cha Jimbo.

Ili kuwezesha uwasilishaji wa matokeo katika Maeneobunge 290, IEBC itatoa nafasi kwa jenereta pamoja na nishati ya gridi ya taifa.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati aliwahakikishia Wakenya kuwa kila kifaa cha KIEMS kina mitambo miwili ya ziada ya kuhifadhi umeme utakaotosha zoezi zima la upigaji kura na uwasilishaji wa matokeo.

 Vituo vyote vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia saa kumi na mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni na endapo kutakuwa na ucheleweshaji, tume ilisema kuwa Msimamizi ataongeza muda wa saa za upigaji kura kwa muda uliopotezwa kutokana na kuchelewa kwa zoezi la upigaji kura.

Kulingana na kanuni za upigaji kura kila mtu kwenye foleni ataruhusiwa kupiga kura hata baada ya kukamilika kwa muda wa kupiga kura.