Raila ampigia debe Ababu wa UDA kimakosa

Raila alinuia kumfanyia kampeni Raphael Wanjala ambaye anawania kiti cha Ubunge wa eneo hilo

Muhtasari

•Wanjala anatafuta kuhifadhi kiti chake tangu alipokinyakua chini ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Raila.

Ababu Namwamba
Ababu Namwamba
Image: HISANI

Aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, alimuidhinisha kimakosa Ababu Namwamba wakati wa kampeni eneo la Budalangi kaunti ya Busia.

Akiwahutubia umati mnamo Jumatano, Agosti 3, Waziri Mkuu huyo wa zamani, anayewania kumrithi Rais Uhuru Kenyatta mnamo Agosti 9, alitangaza jina la Namwamba kabla ya kujirekebisha haraka.

Raila alinuia kumfanyia kampeni Raphael Wanjala ambaye anawania kiti cha Ubunge wa eneo bunge hilo katika Uchaguzi Mkuu ujao.

"Hapa Budalangi, ni Ababu Namwamba! Hapana! Ni Raphael Wanjala," alitangaza Waziri Mkuu huyo wa zamani huku umati ukishangilia.

Uidhinishaji wake ulikuja muda mfupi baada ya kudai kuwa Namwamba alimsaliti baada ya yeye (Raila) kumsaidia Amwamba aliyekuwa Katibu Mkuu wa Tawala wa Masuala ya Kigeni kukua kisiasa.

Katika hotuba yake, Raila alimlinganisha Namwamba na fisi wa methali ambaye alikwama njia panda wakati wa uwindaji.

"Ababu amechanganyikiwa. Alikuwa mtetezi wangu na nilimlea hadi kwenye nafasi ya CAS. Alipotoka, alitazama upande wa pili na kuona malisho ya kijani.''

"Nilimwambia aende  tu huko, atakapo potea ajilaumu tu  mwenyewe, mimi sina tatizo na hilo," Waziri Mkuu huyo wa zamani alieleza.

Wanjala anatafuta kuhifadhi kiti chake tangu alipokinyakua chini ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Raila.

Ababu aliyekuwa CAS, ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa ODM, alijiondoa katika chama hicho Julai 2016 baada ya kuushtumu uongozi wake kwa kumsaliti.