Mudavadi ni mwanangu, nitampa kazi - Raila

Raila aliahidi kuunda serikali yake akimjumuisha Mudavadi.

Muhtasari

• Raila na Mudavadi walitofautiana baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

• Mudavadi alikuwa mmoja wa vinara wa NASA, pamoja na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.

• Raila alisema alijaribu kumvuta Mudavadi upande wake, lakini kiongozi huyo aliogopa sana kujiunga na upande wake. 

Raila Odinga
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Mgombea urais wa chama cha Muungano wa Azimio – One Kenya Raila Odinga sasa anasema iwapo atachaguliwa Agosti 9, atamjumuisha kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi katika serikali yake. 

Raila alisema Mudavadi ni kama mtoto wake na ameahidi kumpa kazi katika serikali ya Azimio. 

"Yeye ni kijana wangu. Tukienda kwa serikali, nitaita yeye," Raila alisema.  

Kiongozi huyo wa ODM alikariri kuwa ana nia ya kujenga serikali yake akimjumuisha Mudavadi. 

Akizungumza wakati wa kampeni huko Vihiga, Raila alisema alijaribu kumvuta Mudavadi upande wake, lakini kiongozi huyo aliogopa sana kujiunga na upande wake. 

Musalia Mudavadi
Musalia Mudavadi

 "Sasa mara hii ingine nikamwambia tuje pande hii. Yeye amekuwa tena na uoga amevurutwa pande ile," Raila alisema. 

Mudavadi alijiunga na muungano wa Kenya Kwanza Januari 23 mwaka huu . Alidai kuwa aliondoka Muungano wa One Kenya Alliance kwa sababu ulikuwa unasukumwa kufanya kazi na Azimio. 

"Kulikuwa na dhana kwamba OKA ilipaswa kuunganishwa na kufanya kazi na mrengo wa Azimio. Lakini ninachoweza kuwambia ni kwamba nimesimama imara na kufanya uamuzi wangu," alisema. 

Viongozi hao wawili (Raila na Mudavadi), walitofautiana baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Mudavadi alikuwa mmoja wa vinara wa NASA, pamoja na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.