(+video) "Kwenda kama unataka kutoka!" Wajackoyah amfokea mgombea mwenza wake

Jumatano, Wamae alifichua kwamba huenda wakavunja urafiki wao kutokana na kile alisema Wajackoyah anampigia debe Raila.

Muhtasari

• Wajackoyah alisisitiza kwamba licha ya madai ya Wamae kwamba anampigia debe Raila, bado yeye yupo debeni katika uchaguzi wa Agosti 9.

Kinara wa chama cha Roots, wakili msomi George Wajackoyah sasa amejitokeza wazi kuzungumzia madai ya mgombea mwenza wake Justina Wamae kwamba anampigia debe mgombea wa Azimio Raila Odinga.

Wajackoyah ambaye alikuwa akizungumza asubuhi ya Alhamis katika kituo kimoja cha runinga humu nchini alisema kwamba azma yake bado ipo pale pale na atakuwa debeni na kupuuzilia mbali madai ya mgombea mwenza wake kwamba anampigia kampeni Raila kisirisiri baada ya video kuvujishwa akimsifia Raila katika kumbi moja ya starehe jijini Kisumu.

Wajackoyah vile vile ameibua madai kwamba anajua kuna wafitinishaji ndani ya chama chake na amekuwa akiwaona ila hawezi kuwafukuza.

“Na ukweli ni kwamba najua niko na wachongaji ndani ya kundi langu, siwezi kuwafukuza. Sasa wanakuja na madai kwamba mimi namsapoti Raila ooh nitamsapoti Ruto. Ni sawa, ni haki yao ya kidemokrasia na hilo halinihusu. Chenye najua ni kwamba mimi nitakuwepo debeni,” Wajackoyah alitema makali ya tanuru.

Profesa huyo wa sheria alisema kwamba hajamshikilia mtu yeyote katika kambi yake kuodoka na kusema yeyote anayetaka kuondoka na kuenda kwa kambi za Raila au Ruto milango ipo wazi kabisa muda wowote wanaweza wakafanya hivyo.

Wajackoyah alitolea mfano kwamba mwaka wa 2012 alirudi nyumbani akapata mamake amevalia nguo yenye nembo ya Mudavadi hali ya kuwa pia yeye alikuwa anawania na alipomuuliza mamake, alimjibu kwamba ni kweli mimi nilikuzaa lakini nampigia upato Mudavadi.

“Ni sawa kama katika mrengo wangu, kama kuna watu wanahisi kwamba wanaweza enda kujiunga na Kenya Kwanza, waende tu. Na kitu mimi najua ni kwamba watu ambao wanaunda sheria na maamuzi katika chama cha Roots wako juu na hawa wanaopayuka hawamo hata kwa kamati ya utendaji,” alisema Wajackoyah.

Mgombea urais wa Roots, George Wajackoyah wakifokeana na mgombea mwenza Justina Wamae
Mgombea urais wa Roots, George Wajackoyah wakifokeana na mgombea mwenza Justina Wamae
Image: Facebook