(+video) Mwaure: baraza langu la mawaziri - Matiang'i, Wajackoyah, Rachel Ruto, Ida Odinga, n.k

Pia aliwapendekeza aliyekuwa jaji mkuu David Maraga, Ruben Kigame miongoni mwa majina mengine.

Muhtasari

• Pia alimtaja mgombea mwenza wa Wajackoyah, Justina Wamae kuwa mmoja katika baraza la mawaziri wa serikali ya Agano.

Mgombea urais kupitia chama cha Agano, David Mwaure amekuwa wa hivi punde kuachia majina ya watu atakaowateua katika baraza lake la mawaziri.

Katika video moja iliyopakiwa kwenye ukurasa wa Twitter wa kituo kimoja cha runinga cha humu nchini, Mwaure anaonekana akitaja majina ya watu kadha, wakiwemo mke wa nqaibu rais wa sasa, Rachael Ruto na pia mke wa kinara wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga, Ida Odinga.

Mwaure alisema kwamba pendekezo hilo la majina ya mawaziri wake iwapo atashinda uchaguzi wiki kesho basi ni ya wakenya ambao wamebarikiwa na vipaji ainati.

"Tumependekeza majina kwa afisi za chama chetu majina ya Wakenya wenye vipaji kutoka sekta zote ikiwemo sekta ya uanahabari, watu ambao watahudumu katika baraza letu la mawaziri, na wacha niwadokezee majina ya wachache ambao tumewapendekeza, katika mawaziri wa sasa majina kama ya Dkt. Matiang'i na Magoha yamependekezwa na zaidi ya mtu mmoja, na majina mengine yatatajwa," alisema Mwaure.

Mgombea urais huyo anayedhaniwa kutokuwa na ufuasi mwingi nchini alizidi kutaja majina ya watu mashuhuri wengi ambao alisema atawashirikisha katika baraza la serikali ya Agano.

"Kutoka kwa dini majina kama yale ya kasisi Askofu Anthony Muheria amependekezwa kuhudumu katika baraza la mawaziri, na sisi tutawaruhusu watu wa dini kufanya kazi kuwili, ndani ya serikali na pia kuhudumu kama watumishi wa Mungu, pia tumepata pendekezo la Mama Winnie Owiti kutoka kaunti ya Kisumu," alisema mwaure katika video hiyo.

Katika kile kinaonekana kama ni utani, Mwaure anasema kwamba pia Alhamis asubuhi wamepokea jina la Justina Wamae ambaye ni mgombea mwenza wa George Wajackoyah na kusema kwamba wameshazungumza na mgombea mwenza wake na kusema ni rafiki yake mkubwa kwa sababu walijadiliana katika mdahalo.

Majina mengine ambayo Mwaure alitaja ni pamoja na jina la aliyekuwa na azma ya kugombea urais Ruben Kigame, aliyekuwa jaji mkuu David Maraga, Ida Odinga, Rachel Ruto,  mwanaharakati Okiya Omtata, PLO Lumumba miongoni mwa wengine wengi .