(+video) "Nilifunga Bukhungu nikawafukuza, hakuna kitu cha bure!" - Gavana Oparanya

Oparanya alifichua kwamba Ruto na mrengo wake walishindwa kulipia Bukhungu akafunga.

Muhtasari

• "Walinitusi lakini nikajua matusi yao hakuna mahali inaenda,” Oparanya alisema.

Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya sasa amefunuka sababu ya kunyima muungano wa Kenya Kwanza kibali cha kufanya mkutano wao katika uwanja wa Bukhungu wikendi iliyopita.

Wikendi iliyopita, muungano wa Kenya Kwanza ukiongozwa na Ruto walitaka kukongamana katika uwanja wa Bukhungu ila wakanyimwa kibali kwa kile waliambiwa kwamba uwanja huo ulikuwa unafanyiwa usafi.

Akizungumza Jumatano katika uwanja huo ambako Raila alifanya kongamano la kampeni zake, Oparanya alisema kwamba alifunga uwanja huo kutotumiwa na Kenya Kwanza kwa kile alisema kwamba muungano huo haukulipia ada ya matumizi kinyume na maneno yao kwamba waliupa uongozi wa kaunti takribani laki 9 ili kutumia uwanja huo.

“Unajua wale jamaa walikuja nikafunga huu uwanja. Nikakataa hawaingii. Nakawaambia waende hakuna kitu cha bure. Walinitusi lakini nikajua matusi yao hakuna mahali inaenda,” Oparanya alisema.

Huku kampeni zikielekea mkumbo w alala salama, wanasiasa katika miungano na mirengo mbalimbali wanazidi kurindima ngoma za sera zao kwa wananchi huku wakitarajiwa kufanya kampeni za mwisho siku ya Jumapili wikendi hii.

Tayari muungano wa Azimio la Umoja One Kenya umetangaza mipango yao ya kukongamana katika uwanja wa kimataifa wa Moi Kasarani jijini Nairobi huku ule wa Kenya Kwanza ukiwa katika njia panda baada ya kudai kwamba kongamano lao lililotarajiwa kufanyika uwanja wa Nyayo, wamenyimwa kibali cha uwanja huo.

Jumatano mmoja wa vinara wa Kenya Kwanza, Moses Wetangula alisema kwamba ikitokea wamezuiliwa kutumia Nyayo basi tayari mipango Madhubuti ishawekwa tayari na watakongamana katikati ya jiji la Nairobi katika makutano ya barabara ya Moi na Kenyatta.