Rais Kenyatta afunguka kuhusu kumiss ikulu baada ya kustaafu

Uhuru alibainisha kuwa ana mahali pa kwenda kuishi hata baada ya kustaafu na kupungia ikulu mkono wa buriani.

Muhtasari

•Rais alikiri kuwa kuna uwezekano mkubwa wa yeye kuwapeza watu ambao amekuwa akihudumu nao katika ikulu.

•Rais alibainisha kuwa ana mahali pa  kwenda kuishi hata baada ya kustaafu na kupungia ikulu mkono wa buriani.

Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta anajiandaa kuondoka Ikulu katika siku zijazo ili kutoa nafasi kwa kiongozi mpya wa taifa ambaye atashinda uchaguzi mkuu wa Jumanne, Agosti 9.

Kenya inatazamiwa kupata rais mpya baada ya Uhuru Kenyarra kukamilisha mihula miwili ambayo katiba inamruhusu kuhudumu.

Akizungumza na jamii ya GEMA kupitia stesheni za eneo hilo mnamo Jumapili usiku, rais alikiri kuwa kuna uwezekano mkubwa wa yeye kuwapeza watu ambao amekuwa akihudumu nao katika ikulu.

"Kuhusu kama nitamiss ikulu, mtu hawezi kosa kumiss. Lakini hii ni nyumba tu, chenye naweza kumiss labda ni wafanyikazi wenzangu tu. Lakini watu tutakuwa tunakutana nao kwenye makanisa, mtaani,  tukienda kula mbuzi pamoja mahali na katika mikutano ya wazee..," rais Uhuru alisema.

Rais alidokeza kuwa kuongoza nchi si kuhusu nyumba ambamo mtu anaishi bali ni kuhusu jinsi gani anavohusiana na watu.

Pia alibainisha kuwa ana mahali pa  kwenda kuishi hata baada ya kustaafu na kupungia ikulu mkono wa buriani.

"Nyumba kwani ni nini? Ata mahali nitaenda, kwani mnadhani Ichaweri sina kitanda? niko na kitanda na kiti. Chenye naweza kusema nitamiss ni watu. Na watu tutakuwa nao tu. La muhimu zaidi ni jinsi mtu anavyohusiana na watu anaoishi nao," Alisema.

Uhuru alitua fursa hiyo kupendekeza kuwepo kwa watu kuishi pamoja na kuhusiana kwa amani na utulivu akisema kuwa kungeifanya nchi kuwa nzuri.

Rais alikuwa akihutubia jamii za Kikuyu, Embu na Meru katika kipindi kilichopeperushwa moja kwa moja kwenye vituo vya eneo la mlima Kenya kutoka ikulu iliyo jijini Nairobi.

Ilikuwa hotuba yake ya mwisho kwa jamii hizo akiwa bado rais wa Kenya kabla ya kustaafu kwake baada ya kukabidhi mamlaka kwa mwingine.