Chebukati awasihi Wakenya kuwa wavumilivu huku matokeo yakianza kutirikika

Hadi saa nne unusu usiku, vituo 26,881 kati ya 46,229 viliwasilisha kwa ufanisi Fomu 34A.

Muhtasari

•IEBC kwa sasa inapokea picha za Fomu 34A kutoka kwa vituo vya kupigia kura na watasubiri stakabadhi halisi kabla ya kuanza kujumlisha.

•Wasimamizi wa Uchaguzi wanatarajiwa kuanza kutoa fomu halisi kuanzia kesho kwa ajili ya zoezi la uhakiki.

akizungumza katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 9, 2022
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati akizungumza katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 9, 2022
Image: ENOS TECHE

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati ametoa wito wa uvumilivu wakati matokeo yanapoanza kutiririka katika kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura.

Mkuu huyo wa IEBC alisema Tume hiyo kwa sasa inapokea picha za Fomu 34A kutoka kwa vituo vya kupigia kura na watasubiri stakabadhi halisi kabla ya kuanza kujumlisha.

Tume imeweka madawati matano ambapo uhakiki wa matokeo yaliyopokelewa utafanyika dhidi ya nyaraka halisi.

Wasimamizi wa Uchaguzi wanatarajiwa kuanza kutoa fomu halisi kuanzia kesho kwa ajili ya zoezi la uhakiki.

"Kama tume tunatoa wito wa uvumilivu miongoni mwa Wakenya tunapofanya zoezi hili kali, tunajitahidi kukamilisha zoezi hili haraka iwezekanavyo," Chebukati alisema.

Hadi saa nne unusu usiku, vituo 26,881 kati ya 46,229 viliwasilisha kwa ufanisi Fomu 34A.

"Katika kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura, tutafanya uhakiki wa picha iliyotumwa ya fomu ya matokeo 34A dhidi ya fomu za awali za 34A," alisema.

Alibainisha kuwa Wakenya wanaweza pia kufuatilia kwenye tovuti ya Tume ili kupata hati za matokeo zinazotumwa kutoka vituo vya kupigia kura.

Akihutubia kikao cha wanahabari usiku wa kuamkia leo, Chebukati hata hivyo alitoa imani kwamba watakamilisha mchakato huo na kutangaza matokeo ndani ya muda wa siku saba wa kikatiba.