Moses Kuria akubali kushindwa katika kinyang'anyiro cha ugavana wa Kiambu

"Nilifurahia kila dakika ya miaka 8 katika siasa za kuchaguliwa. Narudi kwenye sekta ya kibinafsi."

Muhtasari

•Kuria alisema sasa anarejea katika sekta ya kibinafsi baada ya miaka minane ya huduma kama mbunge.

•Tangazo lake lilijiri hata kabla ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutangaza matokeo ya mwisho ya kiti chochote.

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria mnamo Jumatano Machi 30, 2022 alipofika mbele ya IEBC Nairobi.
Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria mnamo Jumatano Machi 30, 2022 alipofika mbele ya IEBC Nairobi.
Image: MAKTABA

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria amedokeza kukubali kushindwa katika uchaguzi wa ugavana wa Kiambu. 

Katika taarifa kwenye Facebook, Kuria alisema anarejea katika sekta ya kibinafsi baada ya miaka minane ya utumishi kama mbunge.

"Nilifurahia kila dakika ya miaka 8 katika siasa za uchaguzi. Narudi kwenye sekta ya kibinafsi. Kwa furaha," Kuria aliandika kwenye Facebook.

Tangazo lake lilijiri hata kabla ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutangaza matokeo ya mwisho ya kiti chochote.

Hapo awali mbunge huyo  aliwahi kuapa kuwa ataachana na siasa ikiwa atashindwa kunyakua kiti cha ugavana wa Kiambu kwenye uchaguzi wa Agosti 9.

"Ikitokea kwamba sijachaguliwa, hutaniona tena katika siasa achilia mbali kutafuta kuteuliwa. Kuna maisha zaidi ya siasa," Kuria alisema katika chapisho la awali la Facebook mnamo Julai 12, 2022.

Kiongozi huyo wa Chama Cha Kazi aliyasema hayo huku akipuuzilia mbali madai kwamba alituma jina lake kwa ajili ya uteuzi wa mbunge kama mpango mbadala iwapo atapoteza kiti cha ugavana.

“Nia yangu moja ni kuchaguliwa kuwa Gavana wa Kaunti ya Kiambu na William Ruto awe Rais,” akasema kwenye wadhifa huo.

Kuria alikuwa akimenyana na Kimani Wamatangi wa UDA, James Nyoro wa Jubilee, William Kabogo wa Tujibebe Wakenya Party , Wainaina wa Jungle (Mgombea huru) , Mwende Gatabaki wa Safina Party na Juliet Kimemia.