Vigogo wa siasa wanaohusishwa na rais Uhuru wafagiwa na wimbi la Ruto Mt. Kenya

Wagombea ubunge wa UDA katika maeneo bunge yote sita ya Nyeri wanatazamiwa kushinda.

Muhtasari

•Jeremiah Kioni ambaye alikuwa alitazamia kutetea kiti chake cha ubunge wa Ndaragwa pia alilambishwa sakafu katika uchaguzi mkuu wa Jumanne.

•Huko Kipipiri, ilikuwa siku ya huzuni kwa Kimunya ambaye alishindwa na mgombea wa UDA Wanjiku Muhia.

Image: FACEBOOK// AMOS KIMUNYA

Wababe wa siasa wanaohusishwa na chama cha Rais Uhuru Kenyatta cha Jubilee walinyenyekezwa na wimbi la UDA katika Mlima Kenya akiwemo kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa Amos Kimunya.

Katibu mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni ambaye alikuwa alitazamia kutetea kiti chake cha ubunge wa Ndaragwa pia alilambishwa sakafu katika uchaguzi mkuu wa Jumanne.

Uchunguzi wa kina umeonyesha kuwa washirika wa Naibu Rais William Ruto katika Mlima Kenya wanaelekea kupata ushindi mkubwa katika viti vya ubunge na ugavana.

“Asante kwa nafasi ya kuwahudumia, imekuwa ni heshima. Ninakubali matokeo kwa kuridhika,” Kioni alisema kwenye ukurasa wake wa Facebook Jumanne mchana.

Mwenyekiti huyo wa kamati ya utekelezaji wa katiba ya Bunge la Kitaifa alizomewa na George Gachagua wa UDA.

Huko Kipipiri, ilikuwa siku ya huzuni kwa Kimunya ambaye alishindwa na mgombea wa UDA Wanjiku Muhia.

Mbunge huyo pia alitumia mitandao ya kijamii kuwashukuru wakazi wa Kipipiri, ambako alihudumu kama mbunge kwa miaka 15.

"Wananchi walifanya uamuzi wao, ambao ulikuwa tofauti na matarajio yetu. Katika demokrasia, matakwa ya watu yanatawala, na kwa hivyo mimi na #TeamKimunya tutaheshimu chaguo lao," Kimunya alisema.

Kufikia Jumatano katikati ya siku, Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga alikuwa mbele ya washindani wake wawili wakuu katika kinyang'anyiro hicho, Thuo Mathenge wa TND na Seneta Ephraim Maina wa Jubilee.

Pia kulikuwa na dalili za wazi kuwa Mwakilishi wa Wanawake Rahab Mukami angehifadhi kiti chake huku Wahome Wamatinga akiwa mbele ya mpinzani wake wa karibu Priscilla Nyokabi wa Jubilee.

Wengine wanaotazamiwa kushinda ni pamoja na wagombea ubunge wa UDA katika maeneo bunge yote sita ya Nyeri.

Miongoni mwa viongozi wanaotarajiwa kupoteza viti vyao katika kinyang'anyiro hicho ni pamoja na Mbunge wa Kieni Kanini Kega, Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), Anthony Kiai (Mukurwe-ini) na Gichuki Mugambi (Othaya).

Mgombea wa UDA Njoroge Wainaina alikuwa mbele ya Kega huku Maina Mathenge akiwa mbele ya Wambugu naye spika John Kaguchia akiongoza katika kinyang'anyiro dhidi ya Kiai.

Mugambi tayari amekubali kushindwa kupitia kwenye ukurasa wake wa Facebook.

"Nachukua fursa hii kuwashukuru watu wa Othaya kwa kunipa nafasi ya kuwatumikia kama Mbunge wao kwa miaka 5 iliyopita," aliandika.

"Sina shaka tumemuacha Othaya bora kuliko tulivyoipata. Nawashukuru wale wote ambao wametembea nami katika safari hii."

Mwingine ambaye yuko tayari kushinda ni MCA wa Konyu Eric Wamumbi ambaye aliteuliwa kuwania kiti cha mbunge wa Mathira kwenye UDA baada ya kinara Rigathi Gachagua kuchaguliwa kuwa mgombea mwenza wa DP Ruto.

Inatarajiwa pia kuwa zaidi ya asilimia 90 ya MCAs wa Nyeri watachaguliwa kwenye UDA.

Baada ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Ruto, Gachagua alifanya ziara nyingi Nyeri, ambapo alimfanyia kampeni mgombeaji wake wa urais na wagombeaji wengine wa UDA ili kuzuia uungwaji mkono wa DP katika eneo hilo.