Waiguru alalamikia wizi wa kura huku hesabu za kura zikiendelea Kirinyaga

Ngirici alieleza imani yake katika mchakato wa uchaguzi.

Muhtasari

•Waiguru alidai kuwa masanduku mawili ya kura yaliingizwa katika kituo cha kuhesabia kura cha Kianyaga.

Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru akipiga kura katika shule ya msingi ya Kiamugumo, kaunti ya Kirinyaga.
Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru akipiga kura katika shule ya msingi ya Kiamugumo, kaunti ya Kirinyaga.
Image: WANGECHI WANG'ONDU

Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru ameibua madai ya wizi wa kura huku ujumuishaji wa kura ukiendelea.

Alidai kuwa masanduku mawili ya kura yaliingizwa katika kituo cha kuhesabia kura cha Kianyaga.

"Wizi wa kura mchana peupe -Sanduku mbili za kura zilizo na karatasi za magavana zimeingizwa Kianyaga kupitia mlango wa nyuma mchana kweupe!"

"Lazima ziondolewe na kuhesabiwa kwa kura lazima kusimamishwe," Waiguru aliongeza.

Gavana huyo anatafuta kutetea kiti chake kwa muhula wa pili kutumia tiketi ya Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Mpinzani wake mkuu, Wangui Ngirici ni mgombea huru.

Siku ya Jumanne, Ngirici alieleza imani yake katika mchakato wa uchaguzi.

Akizungumza katika kituo cha kupigia kura cha Kaitheri Polytechnic, mjini Kerugoya muda mfupi baada ya kupiga kura, mgombeaji huyo wa kujitegemea alliwataka wafuasi wake kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuleta mabadiliko.

Alitaja zoezi hilo kuwa la kuleta mabadiliko na kuwataka wapiga kura kutekeleza wajibu wao wa kiraia kwa busara.