Wetangula awachachafya wana DAP-K, Kura nyingi Bungoma Zikienda kwa Ruto

Ford Kenya yawarudisha nyumbani maadui wa kisiasa Wamunyinyi na Eseli.

Muhtasari

• Wamunyinyi na Eseli ni miongoni mwa waliopigiwa upatu na wagombeaji wa Ford Kenya.


• Walikuwa Ford Kenya kabla ya kukosana na Wetang’ula na kujiunga na DAP-K.

Moses Wetangula
Moses Wetangula

Kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetang’ula amewashinda washirika waliogeuka kuwa maadui Wafula Wamunyinyi (Kanduyi) na Eseli Simiyu (Tongaren) katika Uchaguzi Mkuu wa Jumanne.

Wamunyinyi na Eseli, ambao ni kiongozi wa chama cha Democratic Action Party of Kenya na katibu mkuu mtawalia, walipoteza viti vyao vya ubunge kwa wagombea wa Ford Kenya katika uchaguzi huo.

Katika kinyang'anyiro cha ubunge wa Kanduyi, John Makali wa Ford Kenya aliibuka mshindi baada ya kupata kura 32,099 dhidi ya kura 20,240 za Wamunyinyi.

Alfred Khangati wa ODM aliibuka wa tatu kwa kura 12,970.

Katika kinyang'anyiro cha Tongaren, John Chikati wa Ford K alimshinda Eseli baada ya kupata kura 20,108. Eseli alisimamia kura 9,802 pekee.

Wamunyinyi na Eseli walikuwa Ford Kenya kabla ya kukosana na Wetang’ula na kujiunga na DAP-K.

Kwa jumla, Wetang’ula aliwasilisha kura za kaunti yake ya Bungoma kwa Naibu Rais William Ruto. Wamunyinyi na Eseli walikuwa wamejaribu kuifanya kaunti hiyo kuwa ngome ya DAP-K.

Matokeo ya muda ya Alhamisi asubuhi yalionyesha Ruto amepata kura 229,409 Bungoma ambazo ziliwakilisha asilimia 63.15 ya kura zilizohesabiwa.

Raila Odinga wa Azimio alikuwa na kura 13,478 ambazo ziliwakilisha asilimia 35.92 ya kura zilizohesabiwa.

DAP-K ni mshirika wa Azimio La Umoja-One Kenya Alliance. Chama hicho kinahusishwa na Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa. Eseli na Wamunyinyi waliiacha Ford Kenya na kujiunga na DAP-K mnamo Desemba mwaka jana.

Wawili hao wamehusika katika vita vya muda mrefu na Wetang'ula kuhusu udhibiti wa Ford Kenya. Wamunyinyi na Eseli walihamia DAP-K na kupokea makumi ya waasi kutoka Ford Kenya.

Migogoro katika Ford Kenya ilianza Mei 2020 baada ya baadhi ya viongozi wake kuamua kumfukuza Wetangula kwa misingi ya utovu wa nidhamu.

Inasemekana kwamba nafasi ya Wetang'ula ilichukuliwa na mbunge wa Kanduyi kama kiongozi wa muda wa chama lakini seneta huyo wa Bungoma alikimbilia mahakamani kusitisha hatua hiyo.

Eseli amemshutumu seneta huyo wa Bungoma kwa kujificha nyuma ya mahakama ili kusalia kama kiongozi wa chama. Haikupita muda Eseli na Wamunyinyi wakaiacha Ford Kenya.

 

Tafsiri: Moses Sagwe