Dadake Raila Odinga atwaa kiti cha mwakilishi wa wanawake Kisumu

Anyang' Nyong'o alihifadhi kiti chake kama gavana wa Kisumu huku Tom Ojienda akichaguliwa kuwa seneta.

Muhtasari

•Ruth alipata kura 304,419 dhidi ya mshindani wake mkuu Valentine Anyango wa chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG) aliyepata kura 80,117.

•Jack Ranguma alishindwa katika jaribio lake la kukinyakua tena kiti cha ugavana wa Kisumu baada ya kushindwa na Anyang' Nyong'o wa ODM.

Aliyekuwa Naibu Gavana wa Kisumu Ruth Odinga, alichaguliwa kuwa mwakilishi wa wanawake wa kaunti.
Aliyekuwa Naibu Gavana wa Kisumu Ruth Odinga, alichaguliwa kuwa mwakilishi wa wanawake wa kaunti.
Image: FAITH MATETE

Mgombea kiti cha mwakilishi wa wanawanake wa Kisumu kwa tiketi ya ODM Ruth Odinga ametangazwa mshindi.

Ruth alipata kura 304,419 dhidi ya mshindani wake mkuu Valentine Anyango wa chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG) aliyepata kura 80,117. Alipigania kiti hicho dhidi ya wagombea wengine watatu.

Rose Auma aliibuka wa tatu kwa kura 36,692. Aliwania kama mgombeaji wa kujitegemea. Mgombea wa UDA Filgona Atieno alikuwa wa tatu kwa kura 7, 825.

Ruth ni dadake mgombea urais wa Azimio Raila Odinga. Kati ya 2013 na 2017, Ruth alihudumu kama naibu gavana wa Kisumu.

Jack Ranguma alishindwa katika jaribio lake la kukinyakua tena kiti cha ugavana wa Kisumu baada ya kushindwa na Anyang' Nyong'o wa ODM.

Ranguma ambaye aliwania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha MDG alishika nafasi ya pili katika kinyang'anyiro hicho kwa kura 100, 600 dhidi ya kura 319, 957 za Nyong'o.

Kinyang'anyiro cha ugavana kilivutia wagombeaji wanne.

Beryl Meso, ambaye ni mgombeaji wa kujitegemea alipata kura 3,383 huku Erick Otieno akimaliza wa mwisho kwa kura 2,705.

Wakili Tom Ojienda amenyakua kiti cha useneta wa kaunti hiyo kwa ushindi mkubwa.Ojienda alipata kura 413,121 dhidi ya mpinzani wake pekee Enos Kudi Okolo wa Jubilee aliyepata kura 15,575. Aliwania nafasi hiyo kwa tiketi ya chama cha ODM.

Seneta wa sasa Fred Outa hakutetea kiti hicho baada ya kupoteza uteuzi wa ODM kwa Ojienda mwezi Aprili.