Khalwale wa UDA Ashinda Useneta Kakamega, Mshindani Ampongeza

Brian Lishenga alikubali matokeo na kumpongeza Khalwale.

Muhtasari

“Ni wazi kuwa Dkt Boni Khalwale  atahudumu kama Seneta wa Kakamega kwa miaka 5 ijayo." - Lishenga.

Aliyekuwa seneta wa Kakamega, Boni Khalwale akisherehekea ushindi
Aliyekuwa seneta wa Kakamega, Boni Khalwale akisherehekea ushindi
Image: Facebook//BoniKhalwale

Brian Lishenga, mwanasiasa aliyekuwa anawania useneta Kakamega kupitia tikiti ya chama cha ODM amekubali matokeo baada ya kushindwa na mwanasiasa mkongwe Boni Khalwale.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Lishenga alikubali matokeo na kumhongera Seneta huyo wa kwanza ambaye safari hii alirudi kwa kishindo kwenye kinyang’anyiro kwa kutumia chama cha UDA.

“Ni wazi kuwa Dkt Boni Khalwale  atahudumu kama Seneta wa Kakamega kwa miaka 5 ijayo. Nampongeza na kumtakia mafanikio katika kuwatumikia wananchi wetu. Ninawashukuru kwa dhati wapiga kura wapatao 200,000 wa Kakamega ambao waliweka matumaini, imani na ndoto zao kwangu, mwanasiasa kijana kwa mara ya kwanza. Nimeheshimiwa sana. Ninawaahidi kuwa #AJENDA_YA_MATUMAINI ya Kaunti ya Kakamega ingali hai na yenye afya tele,” Lishenga alisema.

Mwanasiasa huyo mchanga pia alizidi mbele kwa kuishukuru familia yake na pia kamati iliyokuwa ikiendesha kampeni zake katika kaunti hiyo yenye wingi wa wapoga kura eneo pana la mkoa wa magharibi.

“Ninaishukuru timu yangu ya kampeni, inayoongozwa na Faith Gitira ambaye ni mahiri asiyechoka, ulinitoa kwenye hali ya kusikojulikana hadi hadhi ya jina la nyumbani kwa muda wa miezi 4 pekee. Hebu tufanye hivi tena muda si mrefu. Naishukuru familia yangu kwa upendo na kujitolea kwenu. Upendo ni kweli mkuu. Sasa nitachukua muda kuungana tena na watoto wangu, kuwatia nguvu tena na kuendelea kutumikia kaunti na nchi yangu kwa njia yoyote inayopatikana na iwezekanavyo,” Lishenga aliendelea.

Boni Khalwale alikuwa mbunge wa Ikolomani baada ya kuchaguliwa kama seneta wa kwanza wa Kakamega, wadhifa ambao aliachia Cleophas Malala mwaka 2017 alipojaribu guu lake la bahati katika kiti cha ugavana ila akashindwa na gavana anayeondoka Wycliffe Oparanya.

Alipata kura 247,860 dhidi ya mshindani wake wa karibu Brian Lishenga aliyepata kura 195,052 na kurudi katika seneti tena kwa mara ya pili.