Migori: Aliyepoteza tikiti ya ODM baada ya kuuza nyumba ya KSh 25M ashinda kama mgombea huru

Fatuma Mohammed aligonga vichwa vya habari April baada ya kuteta kudhulumiwa na ODM katika uchaguzi wa mchujo wa chama

Muhtasari

• :Wananifanyia mabaya, napiga magoti na kusema ‘ni sawa Baba’. Lakini kwa nini mimi? Kwanini mimi?" - Fatuma alilalama kipindi hicho.

Fatuma Mohammed
Fatuma Mohammed
Image: Screengrab//YouTube

Fatuma Mohammed, ni mwanasiasa kutoka kaunti ya Migori aliyegonga vichwa vya habari baada ya kudai kwamba amenyimwa tikiti ya chama cha ODM kuwania uwakilishi wa kike hata baada ya kutumia mamilioni ya pesa kwenye kampeni za mchujo, pesa ambazo alidokeza kwamba aliuza nyumba yake ya kifahari kwa shilingi milioni 25 pesa za Kenya.

Mohammed sasa ametangazwa kuwa mwakilishi wa kike mpya kabisa kweney kaunti hiyo baada ya kuamua kuwania kama mgombea huru kwa kile alisema kwamba chama cha ODM kilimdhulumu katika chaguzi za mchujo kwenye kaunti ya Migori.

Mnamo mwezi April, Fatuma Mohammed alilia vikali mbele ya vyombo vya habari akisema kwamba chama hicho kilianza kumdhulumu uchaguzi wa 2013 ila akawa anaywea tu na kuahidi kwamba safari hii hangevumuilia tena na ndio maana aliamua kujitupa uwanjani kama mgombea huru.

“Nimekuwa mnyenyekevu wa haki sana kwa chama. Wananifanyia mabaya, napiga magoti na kusema ‘ni sawa Baba’. Lakini kwa nini mimi? Kwanini mimi? Ninatumia mamilioni. Niliuza nyumba yangu yenye thamani ya milioni KSh 25 ili kuthibitisha kuwa nataka kuwa Mwanamke mwakilishi wa Kaunti ya Migori, na nimedhihirisha hilo, niliteuliwa na chama, walinipa cheti kutokana kwa kura nyingi za umaarufu,” Fatuma Mohammed alilalama kipindi cha uchaguzi wa mchujo.

Ushindi wa Ijumaa asubuhi ulitangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa kaunti, ambaye alisema Mohamed alipata kura 154,538 akifuatiwa na mgombeaji wa ODM Ghati Denittah, aliyepata kura 117,591.