Wetang’ula awaaibisha wanachama waliomtema kwenda DAP-K

Waasi wa Ford Kenya katika kaunti ya Bungoma wamelipa gharama kubwa huku wakipoteza viti.

Muhtasari

•Wanasiasa wa Bungoma waliojaribu kumpindua Wetang’ula kutoka usukani wa Ford Kenya mnamo Mei 2020 wamepoteza.

•Matokeo ya awali siku ya Alhamisi yalionyesha kuwa Lusaka alikuwa anaelekea kushinda kiti cha ugavana Bungoma.

Kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula akizungumza mjini Lokichar, kaunti ya Turkana mnamo Julai 9, 2022.
Kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula akizungumza mjini Lokichar, kaunti ya Turkana mnamo Julai 9, 2022.
Image: MAKTABA

Vigogo wa kisiasa katika kaunti ya Bungoma waliojaribu kumpindua Seneta Moses Wetang’ula kutoka usukani wa Ford Kenya mnamo Mei 2020 wamelipa gharama kubwa.

Wanasiasa hao waliojitoa na kujiunga na Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) baada ya mapinduzi kufeli, wamepoteza viti vyao kwa wagombea wa Ford Kenya.

Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati, wabunge Wafula Wamunyinyi (Kanduyi) na Eseli Simiyu (Tongaren) walijaribu kumtimua Wetang’ula kutoka Ford Kenya wakisema hana uwezo wa kuendesha masuala ya chama.

Watatu hao walimshutumu Wetang’ula kwa kuendesha Ford Kenya "kama kioski chake cha kibinafsi."

Kisha walijiunga na chama cha DAP-K ambacho kinahusishwa na Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa. Wamunyinyi alichaguliwa kuwa kiongozi wa chama hicho na Eseli akafanywa katibu mkuu.Kabla ya uchaguzi wa Agosti 9, Wetang’ula alimuunga mkono mpinzani wake wa zamani, Spika wa Seneti Ken Lusaka, katika azma yake ya kunyakua kiti cha ugavana wa Bungoma kwa tikiti ya Ford Kenya.

Matokeo ya awali siku ya Alhamisi yalionyesha kuwa Lusaka alikuwa anaelekea kupata ushindi.

Mnamo Juni 1, Wangamati alipiga hatua ya kukutana na Wetang’ula na kumsihi kufikiria kuzika ugomvi wao.

Alisema tofauti na Wetang’ula zilidhoofisha utendakazi wake. Alieleza kuwa miradi ya maendeleo imeathirika kwa sababu ya ushindani wao.

"Wetang'ula anafaa kukomesha tofauti zake nami kwa vile tunatoka eneo bunge moja," alisema wakati wa sherehe za kuadhimisha Siku ya Madaraka.

“Wapinzani hawajawahi kuniruhusu kufanya kazi kwa watu wa Bungoma. Kila siku, kila wiki, kila mwezi wanasema jambo la kuchafua jina langu.”

Wetang’ula alimuunga mkono Wangamati mwaka wa 2017 kupitia Ford Kenya lakini wawili hao walitofautiana muda mfupi baadaye.

Wamunyinyi na Eseli pia walipoteza viti vyao.

Katika kinyang'anyiro cha ubunge wa Kanduyi, John Makali wa Ford Kenya aliibuka mshindi baada ya kupata kura 32,099 dhidi ya kura 20,240 za Wamunyinyi.

Alfred Khangati wa ODM aliibuka wa tatu kwa kura 12,970.

Katika kinyang'anyiro cha Tongaren, John Chikati wa Ford Kenya alimshinda Eseli baada ya kupata kura 20,108. Eseli alipata kura 9,802 pekee.

Kwa jumla, Wetang’ula aliwasilisha kaunti yake ya Bungoma kwa Naibu Rais William Ruto.

Wamunyinyi na Eseli walikuwa wamejaribu kuifanya kaunti hiyo kuwa ngome ya DAP-K.

Wamunyinyi na Eseli walikuwa wamejaribu kuifanya kaunti hiyo kuwa ngome ya DAP-K.

Matokeo ya awali Alhamisi asubuhi yalionyesha Ruto amepata kura 229,409 katika kaunti ya Bungoma ambazo ziliwakilisha asilimia 63.15 ya kura zilizohesabiwa.

Raila Odinga wa Azimio alikuwa na kura 13,478 ambazo ziliwakilisha asilimia 35.92 ya kura zilizohesabiwa.

DAP-K ni mshirika wa Azimio la Umoja-One Kenya Coalition.

Wetang’ula na mwenzake wa ANC Musalia Mudavadi walikuwa wameahidi kuwasilisha asilimia 70 ya kura za Magharibi kwa Naibu Rais.

Walitwikwa jukumu la kuwasilisha kura katika kaunti zote za Kakamega, Bungoma, Vihiga, Busia na Trans Nzoia.

Walijadiliana kupata asilimia 30 ya serikali ikiwa muungano wa Kenya Kwanza utatwaa uongozi.Hata hivyo, Mudavadi alishindwa kuwasilisha kaunti yake ya Vihiga, kulingana na matokeo ya muda kwani Raila alikuwa na kura 85,995 (asilimia 59.81) huku Ruto akipata kura 56,283 (asilimia 39.15).

Matokeo pia yalionyesha kuwa Ruto alipata asilimia 76 ya kura zote zilizopigwa katika kituo cha Wetangula katika Shule ya Msingi ya Namakhele, akimshinda mpinzani wake Raila kwa kura nyingi.

Kiongozi huyo wa Ford Kenya na mwenzake wa Amani National Congress walitengana na Raila baada ya kujitenga na muungano wa National Super Alliance ambao sasa umedorora kwa madai ya usaliti wa Waziri Mkuu huyo wa zamani.

Ruto alipata kura 276 katika Shule ya Msingi ya Mululu ambapo kiongozi huyo wa ANC alipiga kura. Raila alipata kura 82 katika kituo hicho cha kupigia kura.

Inasemekana kwamba nafasi ya Wetang'ula ilichukuliwa na mbunge wa Kanduyi kama kiongozi wa muda wa chama lakini seneta huyo wa Bungoma alikimbilia mahakamani kusitisha hatua hiyo.

Eseli amemshutumu Seneta wa Bungoma kwa kujificha nyuma ya mahakama ili kusalia kama kiongozi wa chama. Haikupita muda Eseli na Wamunyinyi wakaiacha Ford Kenya.