Nakuru yaweka historia huku wanawake wakinyakua nyadhifa 8 za uongozi

Kihika alimshinda Gavana wa sasa Lee Kinyanjui wa Jubilee Party ambaye alipata kura 225,623.

Muhtasari

•Siku ya Ijumaa, Seneta wa Nakuru anayeondoka Susan Kihika alitangazwa kuwa gavana mteule wa kaunti hiyo.

•Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia ya Keroche Tabitha Karanja ametangazwa kuwa seneta mteule.

Gavana mteule wa Nakuru Susan Kihika akipokea cheti chake baada ya kumwangusha Gavana wa sasa Lee Kinyanjui.
Gavana mteule wa Nakuru Susan Kihika akipokea cheti chake baada ya kumwangusha Gavana wa sasa Lee Kinyanjui.
Image: JEPTUM CHESIYNA

Nakuru imeweka historia kwa kuwa kaunti ya kwanza kupigia kura idadi kubwa zaidi ya wanawake katika nyadhifa nane za uchaguzi.

Tangu 2013, Kenya imeshuhudia viongozi wengi wanaume katika kaunti zote, hali ambayo kaunti hiyo ya Bonde la Ufa sasa imevunja.

Siku ya Ijumaa, Seneta wa Nakuru anayeondoka Susan Kihika alitangazwa kuwa gavana mteule wa kaunti hiyo.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ilisema alishinda baada ya kupata kura 440,707.

Kihika alimshinda Gavana wa sasa Lee Kinyanjui wa Jubilee Party, aliyepata kura 225,623.

Kihika aliwapongeza wapiga kura kwa kukumbatia uwezeshaji wa wanawake.

“Ninataka kuwashukuru wenyeji wa Nakuru kwa kuwa na maendeleo na kuwachagua wanawake watatu katika uongozi wa kaunti hii,” Kihika alisema.

Wakili huyo ambaye amekuwa katika siasa tangu 2013, alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa spika wa bunge la kaunti ya Nakuru.

Alihudumu hadi 2017 kisha akawania na kushinda nafasi ya useneta ambapo alishinda kwa kura 637,700.

Kwa nafasi ya kiti cha useneta, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia ya Keroche Tabitha Karanja ametangazwa kuwa mshindi.

"Hii ni kaunti ya kwanza ambayo imechagua wanawake wengi na hatutawaangusha wanawake wa Nakuru. Tutadhihirishia ulimwengu kuwa wanawake wanaweza kufanya vyema zaidi ya vile wanaume wanaweza kufanya," alisema.

Msimamizi wa uchaguzi katika kaunti ya Nakuru Joseph Melle alisema Karanja alishinda kwa kura 442,864.

Alimshinda aliyekuwa bosi wa NACADA, John Mututho, ambaye alipata kura 36,432.

Alikuwa akichuana na wapinzani wengine wanne, akiwemo Gachinga Mwai (7,223), Koigi Wamwere (6,335), Githenya Mwangi (4,680) na Lawrence Karanja (163).

Mjasiriamali huyo aligombea kwa tiketi ya UDA.

Liza Chelule alihifadhi kiti chake cha uwakilishi wa mwanamke baada ya kupata kura 382,143. Mshindani wake wa karibu, Agnes Njambi wa Jubilee Party, alipata kura 194,610.

Maeneobunge manne kati ya 11 ya kaunti hiyo pia yamechagua wanawake.

Irene Njoki wa Jubilee alinyakua kiti cha Mbunge wa Bahati huku mwenzake wa Naivasha, Jane Kihara wa UDA, akichaguliwa tena.

Wengine ni pamoja na Martha Wangari wa UDA wa Gilgil na Charity Kathambi aliyeshinda kiti cha ubunge cha Njoro.

Kiti cha MCA cha Bahati pia kilimwendea mwanamke, Grace Mwathi.