Osoro - Haikuwa rahisi, mlinichagua bila kupokea hata bob kutoka kwangu, ahsante South Mugirango!

Hapa vita ilikuwa ni mimi dhidi ya watu wengi (majina) - Osoro

Muhtasari

• "Ahsante sana ndugu zangu, kura 25,000 si jambo dogo na hamkupata hata shilingi kutoka kwangu,” Osoro alisema.

Mbunge mteule wa South Mugirango, Slyvanus Osoro
Mbunge mteule wa South Mugirango, Slyvanus Osoro
Image: Facebook//Slyvanus Osoro

Mbunge wa Mugirango ya Kusini Slyvanus Osoro amewashukuru wakaazi wa eneo bunge hilo lililopo kaunti ya Kisii kwa kumchagua kwa mara nyingine tena licha ya kile alikitaja kwamba majeshi mengi yalikuwa yamehamasishwa kusimama dhidi yake katika eneo bunge hilo.

Akitoa shukrani kupitia ukurasa wake wa Facebook baada ya kupokezwa cheti cha ushindi, Osoro ambaye ni mtetezi mkali wa sera za naibu rais William Ruto na ambaye alikuwa anawania kupitia chama cha UDA alisema kwamba washindani wake walikuwa wengi na walikuwa wameshirikiana na vyombo vya dola pamoja na Waziri Matiangi katika kuwezesha njama ya kumbwaga chini ila wananchi wakasimama tisti na kumchagua kwa wingi licha ya kutopata hata shilingi moja kutoka kwake, ikilingalishwa na washindani wake ambao alisema waliweka watu wa kuwarubuni wapiga kura na pesa katika vituo vya kupiga kura ili kutompigia Osoro.

“Hii nayo wasee haikuwa rahisi.Hata kama nimepiga majamaa kabisa na tofauti kubwa, tofauti na uchaguzi wa awali, hapa vita ilikuwa ni mimi dhidi ya watu wengi (majina), waliweka bajeti ya 500k katika KILA KITUO CHA KURA..watu walikuwa wakipewa pesa na machifu waliokuwa wamevalia sare na kulindwa na Askari, Yaani Kila njama iliwekwa kwa meza.. lakini wapi,” Osoro alisherehekea.

Osoro alisema wafuasi wake kumpigia kura elfu 25 si kitu rahisi pamoja na kumchagua diwani mmoja kwa UDA na wengine wawili kutoka vyama tanzu vya Kenya Kwanza si kitu rahisi.

“Lakini Mungu ni nani, watu walikula pesa, wakaingia kwa vituo vya kupiga kura na kumpigia chaguo lake ambaye ndio mimi. Ahsante sana ndugu zangu, kura 25,000 si jambo dogo na hamkupata hata shilingi kutoka kwangu,” Osoro alisema.