"Msiwe na wasiwasi kwa lolote, bali sali na kuomba" DP Ruto anukuu Biblia

Ruto alinukuu kitabu cha Wafilipino mlango wa nne, mstari wa nne hadi saba

Muhtasari

“Upole wenu na udhihirike kwa watu wote" - Ruto alinukuu.

Naibu rais William Ruto na waumini baada ya ibada Karen
Naibu rais William Ruto na waumini baada ya ibada Karen
Image: Facebook//WILLIAM RUTO

Naibu rais William Ruto Jumapili baada ya kumalizika kwa ibada ya kanisa iliyoandaliwa katika makazi rasmi ya naibu rasmi eneo la Karen, Nairobi aliachia ujumbe mzuri wa kuhimiza kwa wafuasi wake huku taifa liisubiri tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC kutoa tamko rasmi kuhusu mshindi wa kinyang’anyiro cha urais.

Ruto kupitia ukurasa wake wa Facebook aliachia ujumbe kutoka kitabu cha Wafilipino kifungu cha nne mstari wa nne hadi saba ambacho kinawahimiza watu kutokuwa na papara bali kuwa wenye Subira katika kila kitu.

“Upole wenu na udhihirike kwa watu wote. Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lo lote, bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu,” Ruto alinukuu maandiko matakatifu huku akionekana kuwa na biblia mkononi.

Awai mshindani wake mkuu Raila Odinga pia alionekana kwa mara ya kwanza kabisa alipohudhuria ibada ya kanisa eneo lilo hilo la Karen akiandamana na baadhi ya viongozi wanaoegemea mrengo wa Azimio la Umoja One Kenya ambapo naye alinukuu maandiko akisema kwamba atatumika kama zana ya kuhubiri amani haswa kipindi hiki macho na maskio yote yanaelekezwa kwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kutangaza mshindi.

Shughuli ya kudhibitisha hesabu za kura za urais ingali inaendelea katika ukumbi wa Bomas kwa siku ya sita sasa tangu kura ziipopigwa Agosti 9 na Chebukati amewakata wakenya kuwa na Subira huku timu yake ikiendelea kuandaa matokeo hayo ya nyadhifa ya juu kabisa katika uchaguzi wa Kenya.