Simameni kidete nyuma ya Raila na mmuombee- Gladys Wanga awahimiza Wakenya

Wanga amewahakikishia wafuasi wa Raila kwamba timu yao ya wanasheria inajiandaa kupinga ushindi wa Ruto.

Muhtasari

•Wanga alisisitiza kuwa kiongozi wa ODM ndiye mshindi halali wa uchaguzi wa Agosti 9 na akaweka wazi kuwa yote hayajaisha.

•Wanga amewahakikishia wafuasi wa Raila kwamba timu yao ya wanasheria inajiandaa kupinga ushindi wa Ruto.

Image: FACEBOOK// GLADYS WANGA

Gavana mteule wa kaunti wa Homa Bay amewataka Wakenya kusimama na mgombeaji urais wa Azimio Raila Odinga na kumuombea.

Katika ujumbe wa kuwafariji wakazi wa Homa Bay, mwakilishi huyo wa wanawake anayeondoka amewahakikishia wafuasi wa Raila kwamba timu yao ya wanasheria inajiandaa kupinga ushindi wa Ruto.

"Kilichojiri jana ni udanganyifu mkubwa katika uchaguzi ambao pia umefananishwa na mapinduzi ya kiraia. Timu yetu ya wanasheria mahiri imetuhakikishia kuwa kasoro, ubovu wa uchaguzi na ukosefu wa uwazi ambao Mwenyekiti Wafula Chebukati aliendesha shughuli za Tume ni za kishindo kiasi kwamba tamko la tangazo haliwezi kusimama," Wanga alisema kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Alisisitiza kuwa kiongozi wa ODM ndiye mshindi halali wa uchaguzi wa Agosti 9 na akaweka wazi kuwa yote hayajaisha.

Wanga alibainisha kuwa pia yeye amekatishwa tamaa na matokeo yaliyotangazwa na Chebukati katika ukumbi wa Bomas mnamo Jumatatu jioni na kudai kuwa bado hajapata ufahamu wa hali halisi.

"Ninafahamu kuwa wengi wenu kwa sasa mnaumia na kuhangaika na kukata tamaa na kukosa uwazi juu ya kile kilichotokea jana. Kama mfuasi hodari wa Baba, ninashiriki kukatishwa tamaa kwenu. Nimeumia kwa kiwango cha kibinafsi sana," Alisema.

Aidha aliitakia baraka nchi ya Kenya na kaunti yake ya Homa Bay huku hali ya wasiwasi ikiwa imetanda nchini kufuatia matangazo ya matokeo ya urais.

"Wakati huo huo, tusimame imara nyuma ya Baba na kumwombea,"

Jumatatu jioni mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alimtangaza Ruto kuwa rais mteule wa Kenya baada ya kuzoa kura 7,176,141  (50.49%).

Raila ambaye alikuwa akiwania urais kwa mara ya tano aliibuka wa pili kwa kura 6,942,930 (48.85%).