Viongozi wa Afrika wampongeza Ruto kwa ushindi

Ramaphosa alisema kwamba anatazamia kufanya kazi pamoja na rais mteule.

Muhtasari

•Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa pia alimpongeza  Ruto na kuonyesha imani kuwa rais mteule atakuwa kiongozi anayeheshimika.

•Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kwa upande wake alimtakia rais mteule heri katika majukumu yake mapya.

Rais mteule William Ruto na mgombea mwenza wake Rigathi Gachagua wanashikilia cheti baada ya kutangazwa huko Bomas of Kenya mnamo Agosti 15, 2022.
Rais mteule William Ruto na mgombea mwenza wake Rigathi Gachagua wanashikilia cheti baada ya kutangazwa huko Bomas of Kenya mnamo Agosti 15, 2022.
Image: ANDREW KASUKU

Kenya iko mbioni kupata serikali mpya baada ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini Wafula Chebukati kumtangaza William Ruto kuwa rais mteule Jumatatu jioni.

Chebukati alimtangaza kiongozi huyo wa Kenya Kwanza mwenye umri wa miaka 55 kama rais mteule baada ya kuzoa kura 7,176,141 kura za mwisho. Hii ilitafsiri hadi 50.49% ya jumla ya kura halali zilizopigwa.

Kufuatia ushindi huo wa kinyang'anyiro cha Agosti 9, baadhi ya viongozi wa mataifa mbalimbali ya Afrika wamejitokeza kumpongeza naibu rais kwa kupanda ngazi na kunyakua kiti cha juu zaidi nchini.

Katika salamu zake za pongezi, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alisema kwamba anatazamia kufanya kazi pamoja na rais mteule.

"Natoa pongezi zangu za dhati kwa Rais Mteule @WilliamSRuto wa Jamhuri ya Kenya. Kenya yenye ustawi na umoja ni sharti muhimu na mchangiaji katika bara lenye ustawi na amani. Tunatazamia kufanya kazi nawe katika kutafuta Afrika tunayoitaka," Alisema kiongozi wa Afrika Kusini.

Rais wa Burundi aliwapongeza Wakenya kwa kudumisha amani wakati wa uchaguzi na kuviomba vyama vya kisiasa kupatana licha ya matokeo ya kura.

"Pongezi zangu za dhati kwa Rais Mteule WilliamsRuto na watu wa Jamhuri ya Kenya kwa kufanya uchaguzi huru, wa haki na wa amani. Tunawahimiza wahusika wote kulinda amani, na mizozo isuluhishwe kwa njia za kisheria zilizopo. Idumu jumuiya yetu," Jenerali Évariste Ndayishimiye alisema kupitia Twitter.

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa pia alimpongeza  Ruto na kuonyesha imani kuwa rais mteule atakuwa kiongozi anayeheshimika.

"Hongera William Ruto kwa kuchaguliwa kwake kama Rais ajaye wa Kenya," Alisema kwenye Twitter.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kwa upande wake alimtakia rais mteule heri katika majukumu yake mapya.

"Pongezi zangu kwa William Ruto, kwa kuchaguliwa kwako kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya. Nakutakia mafanikio mema katika juhudi zako," alisema.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, rais wa Tanzania Samia Suluhu na rais wa zamani wa Somalia Mohammed Farmaajo pia walimpongeza rais mteule kwa ushindi.