Mike Sonko: Nilipata E Katika Somo la Hisabati

Sonko alisema hata kama alipata E lakini hawezi fanya hesabu mbovu kama Julian Cherera

Muhtasari

• Sonko alikuwa akimtupia tope naibu mwenyekiti wa IEBC Julian Cherera kutokana na takwimu alizosoma vibaya.

Aliyekuwa gavana wa Nairoi, Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairoi, Mike Sonko
Image: Facebook//Mike Sonko

Aliyekuwa gavana wa Nairobi mkwasi Mike Sonko ameendeleza mashambulizi yake ya cheche kali dhidi ya makamishna wanne wa tume ya IEBC waliojitenga na tume hiyo kwa madai kwamab baadhi ya michakato ya kutoa matokeo ya uchaguzi wa urais yalikumbwa na kiza.

Jumanne, makamishna hao wanne waliitisha mkutano wa pili na wanahabari ambapo walitamka takwimu kinzani na za kutatanisha ambazo ziliwafanya kujitenga na mchakato huo, takwimu ambazo Wakenya walizua mjadala mitandaoni kutokana na kwamba zilikuwa haziko sawa kama ambavyo makamishna hao walikuwa wanajaribu kuzisoma.

Wakiongozwa na naibu mwenyekiti wa IEBC Julian Cherera, makamishna hao walisoma takwimu zilizokanganyikana vikali na hivyo kunganganya matamshi yao yenyewe, jambo lililowaacha wakenya wakizungumza katika makundi kuhusu takwimu zao ambazo baadhi walisema zilikuwa si sawa.

Sonko alikuwa mmoja wa wale waliowarushia makamishna hao cheche huku akisema kwamba hata kama yeye alipata alama hasi ya E katika somo la hisabati shuleni lakini hawezi kutoa takwimu si sahihi kama ambavyo mrengo wa Cherera ulifanya.

“Nilipata E katika Hisabati lakini naweza kufanya hesabu bora kuliko huyu memsap wa Sultan (Ali Hassan Joho). Acha kupotosha na kuwalisha wakenya habari za uongo kwa kukosa hesabu rahisi. Unataka Wakenya waamini kuwa 0.01% ni sawa na 140,000?” Sonko aliuliza.

Sonko alikuwa ameidhinishwa na chama cha Wiper ambacho ni moja ya vyama tanzu vilivyounda muungano wa Azimio, kuwania ugavana Mombasa lakini tume ya IEBC ikamkatalia na kumfungia nje kwa kile walisema bado kesi yake ya kubanduliwa kama gavana wa Nairobi ilikuwa haijakamilika.

Sonko aliamua kugura mrengo huo na kujiunga na mrengo wa Kenya Kwanza wiki mbili kuelekea uchaguzi mkuu, kambi ambayo baadaye ilitangazwa kushinda kiti cha urais.