Mutahi Ngunyi: Mei, Nilionya Azimio kuwa 'Deep State' Haingewapa Ushindi, Hawakunisikia

Ngunyi alisema Azimio wana kesi nzuri ila wakizembea mahakamani watavuna mabua

Muhtasari

• “Azimio wana kesi nzuri. Lakini wanamsomea ushairi mtu aliyeshika upanga" - Ngunyi

Mjuzi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa Mutahi Ngunyi ambaye kwa muda mrefu amekuwa akionekana kuegemea mrengo wa Azimio la Umoja One Kenya sasa anaonekana kuyumba na pengine kuachana na mrengo huo.

Ngunyi kupitia ukurasa wake wa Tweeter amefichua kwamba mnamo mwezi Mei, aliwaonya viongozi wa Azimio kwamba Deep State haingeingilia matokeo ya uchaguzi kwa njia yoyote ile na pengine kumsaidia kinara wao Raila Odinga kushinda kama ambavyo wengi walivyokuwa wakiota ndoto hizo nzuri kulingana na yeye.

Alisema kwamba aliwatahadharisha kutotegemea mradi wa masilahi yaani ‘System’ ili kuibuka washindi katika kinyang’anyiro hicho na kuwaambia kwamba mshindani wao mkubwa ambaye alikuwa William Ruto hakuwa mtu rahisi hivyo kama walivyokuwa wakidhani bali ni mtu mweney mikakati kabambe na iliyostawi kisiasa kwa muda mrefu.

Ngunyi aidha alisema kwamba kwa sababu tayari Ruto ashatangazwa mshindi na tume ya IEBC, inawabidi Azimio waelekee katika mahakama ya upeo wa juu ili kuwasilisha kesi ya kutaka ushindi wa Ruto kubatilishwa ila pia ameonya kwamba hata kama wana malalamishi mazuri kisheria lakini iwapo wataendekeza uzembe mahakamani basi watavuna mabua.

“Azimio wana kesi nzuri. Lakini wanamsomea ushairi mtu aliyeshika upanga. Niliwaonya mwezi mei kwamba dola ya masilahi (deep state) haitawasaidia kuleta ushindi. Uvivu kwenye mahakama ya juu utakuwa msala mkubwa kwa upande wao,” Ngunyi alisema.

Mchambuzi huyo aliyejulikana pakubwa kutokana na uchambuzi wake wa jeuri ya idadi ya wapiga kura kwa kimombo ‘Tyranny of Numbers’ alizidi kusema kwamba iwapo Dkt. Ruto alishinda kwa haki basi hana budi ila kuapishwa na kuliendesha taifa mbele na pia kusisitiza kama kulikuwepo na muingiliano wa matokeo na tume ya IEBC basi ni sharti walioshiriki katika mchakato huo kushtakiwa.

“Kenya kwanza, lakini haki kwanza. Iwapo ruto atashinda ipasavyo, kenya itasonga mbele. Iwapo kulikuwa na ujambazi katika iebc, ni lazima turekebishe kwa ajili ya kenya. Kisha best man atashinda. Ni hiyo rahisi,” Ngunyi alalonga, huku safari hii akionekana kuzungumza pasi na kuegemea mrengo wowote.