logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Gavana Kibwana wa Makueni agura Azimio na kujiunga kambi ya rais mteule Ruto

"Gavana wa Makueni atajiunga na timu ya wanasheria wa Kenya Kwanza katika ombi linaloendelea la kupinga uchaguzi wa urais." - Ruto.

image
na Davis Ojiambo

Uchaguzi23 August 2022 - 11:15

Muhtasari


  • • "Katika Makazi ya Karen, nimemkaribisha Gavana Kibwana mrengo wa Kenya Kwanza akiandamana na viongozi wengine," Ruto alidokeza
Rais mteule alimkaribisha gavana anayeondoka wa Makueni katika Kenya Kwanza na kusema ataungana na timu ya wanasheria kutetea ushindi wake katika mahakama ya upeo.

Huku wimbi la wanasiasa nchini Kenya wakionekana kuwa na uchu wa kujiegemeza na upande wa serikali ijayo ambayo tayari tume ya uchaguzi na mipaka IEBC imemtangaza William Ruto licha ya ushindi wake kupingwa mahakamani na mshindani wake Raila Odinga, wanasiasa wengi waliokuwa mrengo wa Azimio la Umoja One Kenya wameendelea kuhama na kujiunga na mrengo wa Ruto.

Wiki jana, vyama na wanasiasa wengi waliokuwa ndani ya muungano wa Azimio pamoja na wale waliokuwa wakigombea kwa tikiti huru walijiunga na Ruto huku suala hilo likizua  tumbo joto miongoni mwa wana Azimio waliosema ni njama ya Ruto kusambaratisha Azimio.

Sasa Ruto ameendeleza kutupa ndoana yake katika baadhi ya viongozi tajika waliokuwa Azimio na ndoana yake safari hii imemnasa gavana anayeondoka wa Makueni msomi wa sheria Kivutha Kibwana ambaye amejiunga Kenya Kwanza.

Akimkaribisha katika makazi yake rasmi huko Karen, Ruto alisema kwamba Kibwana na viongozi wengine kutoka kaunti ya Makueni sasa ni rasmi miongoni wa timu kubwa ya Kenya Kwanza na kudokeza kwamba msomi huyo wa sheria sasa atajiunga katika timu ya mawakili watakaotetea ushindi wa Ruto katika mahakama ya upeo kwenye kesi ambayo iliwasilishwa jana na muungano wa Azimio la Umoja.

"Gavana wa Makueni atajiunga na timu ya wanasheria wa Kenya Kwanza katika ombi linaloendelea la kupinga uchaguzi wa urais. Katika Makazi ya Karen, nimemkaribisha Gavana Kibwana mrengo wa Kenya Kwanza akiandamana na viongozi wengine," Ruto alidokeza kwenye Facebook yake.

Aidha, naibu rais huyo anayeondoka alisema kama Kenya Kwanza wanajivunia maendeleo ambayo gavana huyo ametekeleza katika kaunti hiyo kwa muda wake wa miaka kumi ofisini.

"Tunashirikiana na uongozi ambao Prof. Kivutha Kibwana amedhihirisha kwa kukubali kufanya kazi nasi katika kuendeleza ajenda ya maendeleo ya nchi yetu," Ruto alisema.

Wiki jana viongozi kadhaa waliogombea kwa tikiti huru kama vile gavana mteule wa Meru Kawira Mwangaza walijiunga kwenye kambi ya Ruto huku pia chama cha UDM kikiongozwa na kiongozi wake Ali Roba ambaye ni seneta mteule wa Mandera walijiunga Kenya Kwanza pia.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved