Hakukuwa na viti vya MCA wa Azimio kwenye hafla ya Sakaja- Alai adai

Alai alisema walikuwa na mwaliko wa kuhudhuria hafla hiyo.

Muhtasari

•Alai aliyechaguliwa kwa tikiti ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) alisema walikuwa wamealikwa kuhudhuria hafla hiyo.

Katika maandalizi ya kumuapisha gavana mteule wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja katika KICC mnamo Agosti 25, 2022.
Katika maandalizi ya kumuapisha gavana mteule wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja katika KICC mnamo Agosti 25, 2022.
Image: Star

Kundi la MCAs wa Azimio La Umoja- One Kenya walilazimika kuondoka kwenye hafla ya kuapishwa kwa Johnson Sakaja kama gavana wa nne wa kaunti ya Nairobi,mwanablogu Robert Alai amedai.

Akihutubia waandidhi wa habari, MCA huyo mteule wa Kileleshwa alisema walilazimika kuondoka kwenye hafla hiyo iliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC) baada ya kubaini kuwa hakukuwa na viti vilivyotengewa MCAs wa Azimio.

Alai aliyechaguliwa kwa tikiti ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) alisema walikuwa na mwaliko wa kuhudhuria hafla hiyo.

"Tulialikwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Sakaja na hivyo tulihudhuria, lakini kulikosekana kwa viti vya kukalia, na haswa wale MCAs wa Azimio ndiyo walikosa viti, kwa hivyo, tulilazimika kuondoka," Alai alisema.

"Ni jambo la kushangaza sana kuapishwa kwa  Rais bila wabunge kupata viti. Tulikuwa zaidi ya 25. Kati ya MCAs 45 wa Azimio. Lakini tunataka kumhakikishia (Sakaja) kwamba kama MCAs wa Azimio, tuko tayari kumuunga mkono." Alai aliongeza.

Sakaja aliapishwa kama gavana wa nne wa Nairobi mwendo wa saa tano asubuhi ya Alhamisi katika ukumbi wa KICC. 

Hakimu Roselyn Aburili ndiye aliyesimamia hafla hiyo.

Mamia ya wageni waalikwa wakiwemo wanasiasa mashuhuri walishuhudia kuapishwa kwa Sakaja moja kwa moja. 

Rais mteule William Ruto ni miongoni mwa wageni waliokuwa wamehudhuria.