"Jaribu kumtimua Wamae uone!" Mrengo wa vijana chamani Roots wamuonya Wajackoyah (+video)

Vijana hao walimtetea Wamae kwamba anadunishwa na kiongozi wa chama.

Muhtasari

• Vijana hao walisema hawakujitokeza kumpigia Wajackoyah kura kwa sababu walidokezwa kwamba alikuwa kibaraka wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

Mrengo wa vijana chamani Roots ukimtetea Wamae
Vijana wa Roots Mrengo wa vijana chamani Roots ukimtetea Wamae
Image: Youtube screengrab

Tofauti kati ya kinara wa chama cha Roots wakili msomi George Wajackoyah na naibu wake Justina Wamae inaendelea kuwa pana huku Wajackoyah akiendelea kumshtumu Wamae kwa kuonekana kushabikia ushindi wa rais mteule William Ruto.

Sasa mfarakano katika chama hicho umechukua mkondo mwingine baada ya vuguvugu la vijana chamani Roots kuingilia kati mgogoro kati ya Wamae na Wajackoyah.

Vijana hao wakiongozwa na Raidon Munoko wameibuka na kufyatua risasi kumtetea naibu kiongozi wa chama dhidi ya kile walichosema ni uonevu kutoka kwa kiongozi wa chama. “Kiongozi wa Chama chetu, Profesa George Wajackoyah yuko kwenye rekodi akisema katiba ya chama iko kichwani mwake, hana kamati yoyote na hivyo hakuna kamati ya nidhamu, inakuwaje basi kusema Justina amekiuka mambo ambayo yako kichwani tu?” kiongozi huyo wa vijana chamani alisaili.

Katika kile kilichoonekana kama kumtetea Wamae, mrengo huo wa vijana chamani Roots ulitoa msururu wa madai dhidi ya Wajackoyah, miongoni mwao yakiwa ni uzushi, ukosefu wa uaminifu, na kumkatisha tamaa Wamae hadharani.

Walizungumzia pia madai ya barua iliyotumwa ikimtaka Wamae kujiwasilisha mbele ya kamati ya nidhamu huku ikisema kwamba alikabidhiwa magari rasmi kutoka kwa chama ili kuzunguka nayo kipindi cha kampeni na pia makazi.

Vijana hao walisema kwamab Wamae ni kijana ambaye anajitegemea na ana magari yake kadhaa pamoja na jumba lake la kifahari na kupuuzilia mbali madai ya barua hiyo kwamba alikabidhiwa vitu hivyo na chama.

“Justina anamiliki magari ya kuinua mizigo kutoka chini, lori la kumwaga vitu lenyewe na malori mengine, kwa mtu kama huyo, anaweza kumudu kununua gari. Je, wanazungumzia magari gani rasmi? Justina anakwenda nyumbani kwake baada ya kampeni, ni malazi gani wanazungumza?" kikao hicho cha vijana kilihoji.

Vijana hao walisema kwamba Wajackoyah aliibuka nambari 3 katika uchaguzi uliokamilika kwa sababu vijana wengi walikataa kujitokeza kumpigia kura kwa sababu walidokezwa kwamba alikuwa mradi wa kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga, jambo lililowafisha moyo kujitokeza kupiga kura.