Mmeonyesha ukomavu ambapo wengine wameshindwa-Mudavadi kwa Malala na Omar

Chama cha ODM kilikishinda chama cha United Democratic Alliance katika kinyang'anyiro cha Mombasa na kuwalaza ANC mjini Kakamega.

Muhtasari
  • Katika kinyang'anyiro cha Kakamega, Fernandes Barasa aliibuka mshindi kwa kura 192,929 huku Malala akiibuka wa pili kwa kura 159, 508
Kinara wa ANC Musalia Mudavadi
Kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi Kinara wa ANC Musalia Mudavadi
Image: Musalia mudavadi/TWITTER

Kiongozi wa chama cha ANC na kinara wa Kenya Kwanza Musalia Mudavadi amewapongeza wagombeaji wa muungano huo katika uchaguzi wa ugavana wa Kakamega na Mombasa kwa kuanzisha mapambano ya dhati.

Katika ujumbe wake wa Twitter siku ya Jumanne, Mudavadi alisema ingawa Cleophas Malala na Hassan Omar walishindwa katika uchaguzi huo, bado wana muda wa kutosha mbele yao kugeuza maandishi.

"Ninawashukuru wenyeji wa Kaunti za Kakamega na Mombasa kwa kujitokeza kuwapigia kura wagombeaji wa Ugavana wa Kenya Kwanza.

Ingawa Cleophas Malalah na Hassan Omar Sarai hawakushinda, walifanya juhudi kubwa. Umri bado uko upande wako. Nyote wawili mmeonyesha ukomavu ambapo wengine wameshindwa. Usikatishwe tamaa na anguko tu, wakati ujao unabaki mkali.Hongera kwa washindi."

Katika kinyang'anyiro cha Kakamega, Fernandes Barasa aliibuka mshindi kwa kura 192,929 huku Malala akiibuka wa pili kwa kura 159, 508.

Katika kinyang'anyiro cha Mombasa, Abdulswamad Nassir alishinda kwa kura 119,083 na kumwangusha Hassan Omar wa UDA aliyepata kura 98,105.

Kinyang'anyiro cha ugavana wa Kakamega kilivutia jumla ya wawaniaji saba.

Chama cha ODM kilikishinda chama cha United Democratic Alliance katika kinyang'anyiro cha Mombasa na kuwalaza ANC mjini Kakamega.

Ushindi huo wa ODM ulileta pigo kwa kambi ya Rais Mteule William Ruto ya Kenya Kwanza ambayo ilianzisha mapambano makali kujaribu kumenyana na muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.