Kalonzo achukuwa karatasi za uteuzi kuania wadhifa wa spika wa Seneti na bunge

Kalonzo ni miongoni mwa watu 15 ambao walikuwa wamechukua karatasi za uteuzi kwa nafasi ya spika wa seneti

Muhtasari

• Makamu huyo wa zamani wa rais pia alikuwa amechukua stakabadhi za kutafuta wadhifa wa spika wa Bunge la Kitaifa na sasa tena ameweka mtego katika seneti.

• Wengine ambao wamechukua karatasi hizo kufikia sasa ni Isaac Aluoch, Jared Oundo, George Bush, Dkt Rodgers Manana, Beatrice Kinyua, Dorothy Kemunto na Jecinta Lesiangiki.

 

KINARA WA WIPER KALONZO MUSYOKA
Image: WILFRED NYANGARESI

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ni miongoni mwa watu 15 ambao wamechukua karatasi za kuteuliwa kuwa spika wa Seneti.

Makamu huyo wa zamani wa rais pia alikuwa amechukua stakabadhi za kutafuta wadhifa wa spika wa Bunge la Kitaifa na sasa tena ameweka mtego katika seneti.

Washirika wa Rais mteule William Ruto, aliyekuwa Gavana wa Kilifi Amason Kingi, na aliyekuwa mgombeaji wa ugavana wa Mombasa Hassan Omar pia walikuwa wamechukuwa stakabadhi hizo kufikia saa tisa kasorobo jioni Jumanne.

Aliyekuwa seneta maalum Isaac Mwaura, ambaye alihudumu katika jopo la spika kwenye bunge lililopita pia amechukua stakabadhi za uteuzi wa spika wa seneti.

Katika Seneti, Kalonzo alikuwa miongoni mwa watu 15 ambao walikuwa wamechukua karatasi za uteuzi kwa nafasi ya spika na wawili kwa nafasi ya naibu spika.

Watu wengine ambao wamechukua karatasi hizo kufikia sasa ni Isaac Aluoch, Jared Oundo, George Bush, Dkt Rodgers Manana, Beatrice Kinyua, Dorothy Kemunto na Jecinta Lesiangiki.

Josephat Mutua, Mohamud Halake, Michael Gichuri na Joshua Boit pia walichukuwa karatasi za uteuzi katika Bunge.

Kwa nafasi ya naibu spika, Maseneta wateule Karungo wa Thangwa (Kiambu) na Kathuri Murungi (Meru) walikuwa wamechukua karatasi.

Hata hivyo, kinyang'anyiro hicho kitajulikana baada ya kujua ni nani kati yao atakuwa amerudisha karatasi kufikia Jumatano, saa nane alasiri.

Karatasi za uteuzi zitakazorejeshwa pia zitachunguzwa ili kuhakikisha kuwa wagombeaji wanaafikia vigezo vya sheria.

Maseneta wateule watamchagua spika mara baada ya kuapishwa siku ya Alhamisi.

Spika mpya atamrithi Ken Lusaka ambaye alichaguliwa kuwa gavana wa Bungoma kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.