Aisha Jumwa alambishwa sakafu katika kinyang'anyiro cha ugavana Kilifi

Mung'aro alishinda ugavana kwa kura 143, 773 huku Jumwa akiibuka wa pili na kura 65, 893.

Muhtasari

•Jumwa ambaye alikuwa akiwania kwa tiketi ya UDA alipoteza kwa mpinzani wake wa ODM Gideon Mung'aro.

Mung'aro alitwaa ushindi baada ya kuzoa kura 143, 773 huku Jumwa akiibuka wa pili na kura 65, 893.

Image: FACEBOOK// AISHA JUMWA

Mbunge wa Malindi anayeondoka Aisha Jumwa Katana amefeli katika jaribio lake la kuwa gavana wa Kilifi.

Kulingana na matokeo yaliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa Kilifi katika Jumamosi asubuhi, Jumwa ambaye alikuwa akiwania kwa tiketi ya UDA alipoteza kwa mpinzani wake wa ODM Gideon Mung'aro.

Mung'aro alitwaa ushindi baada ya kuzoa kura 143, 773 kutoka vituo vyote vya kupigia kura vya kaunti hiyo huku Jumwa akiibuka wa pili na kura 65, 893.

George Kithi wa PAA aliibuka wa tatu kwa kura 64,326.

Mung'aro sasa anachukua usukani kutoka kwa Amason Kingi ambaye amehudumu kwa mihula miwili.

Hii ilikuwa mara yake ya pili kwa kujaribu kiti cha ugavana wa Kilifi.

Alishindana kwa mara ya kwanza 2017 lakini hakufanikiwa kumtimua gavana anayeondoka Amason Kingi. 

Kingi ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha ODM alikihama chama hicho na kuunda PAA, ambayo sasa inashirikiana na DP William Ruto. 

Jumwa pia alijiondoa ODM na kujiunga na UDA ya Ruto lakini hakuweza kumshinda mgombeaji wa ODM. 

Alichaguliwa kwa mara ya kwanza kama Mbunge wa Kilifi Woman Rep kwa tikiti ya chama cha ODM mnamo 2017.