Mahakama yamruhusu Ruto kuandaa mkutano wa mwisho Nyayo Stadium

Ruto alichukua hatua za kisheria baada ya idara ya michezo kumzuia kufanya mkutano

Muhtasari

•Ruto hatimaye amepewa mamlaka ya kufanya mkutano wake wa mwisho katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo.


Naibu rais na kiongozi wa Kenya Kwanza
Naibu rais na kiongozi wa Kenya Kwanza
Image: William Samoei Ruto (Facebook)

Mgombea urais wa Kenya Kwanza William Ruto hatimaye amepewa mamlaka  ya  kufanya mkutano wake wa mwisho katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo.

Agizo  la mahakama lilitolewa na Jaji Joseph Sergon baada ya Naibu Rais Ruto kuchukua hatua za kisheria dhidi ya idara ya michezo akipinga uamuzi wao wa kumzuia yeye na timu yake kufanya mkutano wao wa mwisho wa kisiasa katika uwanja wa Nyayo.

Hapo awali, Idara ya michezo inayosimamia viwanja  ilimweleza Ruto, kwamba ukumbi huo tayari ulikuwa umetengwa kwa hafla nyingine mnamo Agosti 6, 2022.

Barua ya maelekezo hayo ilitumwa kwa katibu mkuu wa chama cha UDA Bi Veronica Maina, na kunakiliwa kwa Katibu wa Baraza la Mawaziri la Michezo Amina Mohamed na Katibu Mkuu Joe Okudo miongoni mwa wengine.

"Tunasikitika kuwajulisha kwamba kutokana na tamasha za amani zilizopangwa kufanyika katika Kituo cha Michezo cha Kimataifa cha Moi- Kasarani na Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo kati ya Agosti 5 hadi 7, 2022. Kituo hicho hakitapatikana kwa matumizi yoyote kando na hizo," ilisoma barua hiyo.

Kupitia kwa mpeperushaji wa bendera wa Kenya Kwanza, chama cha UDA kilionyesha kibali kilichodhibitisha  kwamba wameruhusiwa kufanya mkutano wao uliopangwa Agosti 6 katika uwanja wa Nyayo.

Kibali hicho ni baada ya kuizuliwa kwake  na timu yake kufanya mkutano wao wa mwisho wa kisiasa katika uwanja wa Nyayo.