Mike Sonko afichua ahadi za Ruto kwake zilizomvutia kwenye Kenya Kwanza

Sonko amegura muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya na kujiunga rasmi na Kenya Kwanza.

Muhtasari

•Sonko alidokeza kuwa masaibu mengi yaliyokumba azma yake ya kuwania ugavana Mombasa ndiyo yaliyomsukuma kuuonyesha mgongo muungano wa Azimio.

•Sonko alidai kujiunga kwake na UDA kutawahakikishia wakazi wa Nairobi na Mombasa nafasi katika serikali ya Ruto ikiwa atatawaa urais katika uchaguzi ujao.

kwenye Kenya Kwanza katika ofisin zake jijini Nairobi mnamo Julai 30, 2022.
Naibu rais Willliam Ruto akimpokea Mike Sonko kwenye Kenya Kwanza katika ofisin zake jijini Nairobi mnamo Julai 30, 2022.
Image: FACEBOOK// WILLIAM SAMOEI RUTO

Huku masaibu chungu nzima yakiendelea kuiandama azma yake kuwania ugavana Mombasa, Mike Sonko sasa amegura muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya na kujiunga rasmi na Kenya Kwanza.

Mgombea urais wa Kenya Kwanza William Ruto alimkaribisha Sonko kwenye muungano wake Jumamosi asubuhi.

"Tunamkaribisha Mike Sonko kwa Kenya Kwanza, timu inayoshinda," Ruto aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Naibu rais aliambatanisha ujumbe wake na picha zinazoonyesha akimpokea Sonko katika ofisi zake jijini Nairobi.

Sonko alithibitisha mpango wake kugura chama cha Wiper  huku akiomba wafuasi wake ushauri kuhusu kujiunga na UDA.

Gavana huyo wa zamani wa Nairobi alidokeza kuwa masaibu mengi yaliyokumba azma yake ya kuwania ugavana Mombasa ndiyo yaliyomsukuma kuuonyesha mgongo  muungano wa Azimio-One Kenya.

"Nyote mnajua nini kimekuwa kikiendelea na jinsi nilivyosukumwa ukutani nikijaribu kufanya niwezavyo kwa ajili yenu watu wangu wa Mombasa. Muda hauko upande wetu na imenilazimu kukaa chini kama kiongozi, nifikirie nini kingefaa kwa watu wangu na nimegundua kuwa nifanye kazi na serikali yenye maono sawa kwa watu wangu kama mimi. na yenye kuwanufaisha. Sio juu ya Sonko sasa, inabidi nifikirie watu wa Mombasa na mustakabali wao," Sonko alisema Jumamosi asubuhi.

Mwanasiasa huyo asiyepungukiwa na utata alidai kujiunga kwake na UDA kutawahakikishia wakazi wa Nairobi na Mombasa nafasi katika serikali ya Ruto ikiwa atatawaa urais katika uchaguzi ujao.

"Zifuatazo ni nafasi zinazotolewa kwangu pamoja na watu wangu kama zilivyonaswa katika makubaliano ya uchumba/MOU; Waziri mmoja katika serikali ya Kitaifa, Makatibu watatu wa wizara katika serikali ya Kitaifa , Mabalozi Wanne, CEC watatu katika kaunti ya Mombasa, Maafisa Wakuu watatu katika Kaunti ya Mombasa, CEC wawili katika kaunti ya Nairobi, Maafisa Wakuu watatu Kaunti ya Nairobi," Alisema.

Sonko alitangaza kuwa atatia saini makubaliano hayo masaa mawili baada ya chapisho lake ikiwa wafuasi wake watamruhusu.

Aidha aliweka wazi kuwa mgombea mwenza wake katika kinyang'anyiro cha ugavana Mombasa, Ali Mbogo ni mmoja wa ambao watanufainika na nafasi alizoahidiwa katika serikali ya Ruto.

Pia alimshukuru kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka kwa kusimama naye katika azma ya kukikalia tena kiti cha ugavana.

"Pia natoa shukurani zangu kwa Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye amekuwa kama ndugu yangu na kuniunga mkono na simtakii kingine ila kheri njema katika shughuli zake zijazo. Nikienda upande wa pili, naenda kwa amani na kuahidi kampeni za amani sio siasa ya chuki wala matusi.," Alisema Sonko.

Siku chache zilizopita, gavana huyo wa zamani alikuwa ametishia kumuunga mkono mgombea ugavana wa Mombasa kwa tiketi ya UDA Hassan Omar iwapo Ali Mbogo hangeidhinishwa kuwania .