Raila kuwasilisha karatasi za uteuzi kwa IEBC leo; Fahamu stakabadhi anazopaswa kuwasilisha

Muhtasari

•Raila anatarajiwa kuwasilisha stakabadhi zake mwendo wa saa nne asubuhi  katika ukumbi wa Bomas of Kenya.

•Jumatatu, Raila ameratibiwa kuzindua manifesto ya muungano wa Azimio La Umoja One Kenya Coalition katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo.

Image: Martha Karua/TWITTER

Mgombea urais wa Azimio La Umoja Raila Amollo Odinga atawasilisha stakabadhi  zake za uteuzi kwa Tume Huru ya Ucaguzi na Mipaka (IEBC) hivi leo.

Raila anatarajiwa kuwasilisha stakabadhi zake mwendo wa saa nne asubuhi  katika ukumbi wa Bomas of Kenya. Hizi ndizo stakabadhi anazotarajiwa kuwasilisha:

Alifika mwendo wa saa nne alfajiri na anatarajiwa kuwasilisha stakabadhi zifuatazo kwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati saa tano asubuhi;

  • Nakala zilizothibitishwa za vyeti vya elimu.
  • Nakala iliyoidhinishwa ya kitambulisho au pasipoti.
  • Picha saizi ya pasipoti, karatasi na nakala ya kompyuta.
  • Barua ya kuachakazi kutoka kwa mwajiri wa zamani.
  • Cheti cha uteuzi kutoka kwa chama kilichosajiliwa.
  • Kanuni za maadili zilizotiwa saini ipasavyo.
  • Sahihi 2,000 kutoka angalau kaunti 24.
  • Ada ya uteuzi Sh200,000.

Kabla ya kuelekea Bomas Raila ameungana na waumini katika Kanisa la All-Saints Cathedral kwa ibada ya kanisa ambayo inatarajiwa kukamilika muda mfupi kabla ya saa nne.

Viongozi mbalimbali wanaomuunga mkono kinara huyo wa ODM wameandamana naye kuhudhuria ibada hiyo.

Baada ya kuwasilisha karatasi hizo kwa IEBC, Raila ameratibiwa kufanya mkutano katika uwanja wa Undugu eneo bunge la Lang’ata.

Kulingana na taarifa ya katibu wa waandishi wa habari wa sekretarieti ya kampeni ya urais ya Raila, Dennis Onsarigo, Waziri Mkuu huyo wa zamani baadae ataondoka kuelekea Nakuru kufanya  mikutano ya kando ya barabara kuanzia saa nane mchana.

Pia ameratibiwa kufanya mkutano katika viwanja vya Mazembe, eneo la Bondeni mjini Nakuru saa kumi jioni.

Jumatatu, Raila ameratibiwa kuzindua manifesto ya muungano wa Azimio La Umoja One Kenya Coalition katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo.

Mgombea urais wa Kenya Kwanza William Ruto aliidhinishwa kuwania urais katika uchaguzi wa Agosti na IEBC siku ya Jumamosi.

Ruto, ambaye mgombea mwenza wake ni Rigathi Gachagua, baada ya kuidhinishwa aliomba tume hiyo kusalia na haki wakati ikitekeleza majukumu yake.

"Nimefurahi kupata cheti kitakachoniwezesha mimi na naibu wangu kushiriki katika uchaguzi wa Agosti. Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejitolea kwa maadili tuliyotia saini... Tuna imani upo kwenye kazi na tutafanya kazi nanyi kwa bidii," alisema.