Wajackoyah ataja maeneo ya Kenya ambayo ananuia kuyafanya mashamba ya bangi

Muhtasari

•Wajackoyah aliidhinishwa Alhamisi baada ya kutimiza mahitaji yote yaliyotakiwa na tume ya kusimamia uchaguzi.

•Wajackoyah alisema anatazamia kufanya maeneo ya  Bunyore, Mlima Kenya, Nyamira na Kisii kuwa maeneo makuu ya kilimo cha Bangi.

Mgombea Urais wa Roots Party George Wajackoyah na mgombea mwenza wake Justina Wamae.
Mgombea Urais wa Roots Party George Wajackoyah na mgombea mwenza wake Justina Wamae.
Image: EZEKIEL AMINGA

Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imemuidhinisha kiongozi wa Roots Party George Wajackoyah kuwania urais katika uchaguzi wa Agosti 9.

Wajackoyah aliidhinishwa Alhamisi baada ya kutimiza mahitaji yote yaliyotakiwa na tume ya kusimamia uchaguzi.

Akizungumza na waandishi baada ya mkutano wake na IEBC, Wajackoyah alitangaza kuwa yupo tayari kuanzisha kampeni zake kote nchini.

"Tutafikia sehemu zote za nchi hii. Tulianza kampeni zetu rasmi Jumatano. Tutafuata sheria na tutaheshimu sheria. Tunaomba wafuasi wetu wasitupe matusi kwa wagombea urais wengine. Mengine mtaambiwa," Wajackoyah alisema.

Kiongozi huyo alisisitiza kuwa anakusudia kuhalalisha matumizi ya bangi kwa minajili ya dawa pindi atakaponyakua urais.

Wajackoyah alisema anatazamia kufanya maeneo ya  Bunyore, Mlima Kenya, Nyamira na Kisii kuwa maeneo makuu ya kilimo cha mmea huo ambao kwa sasa ni haramu hapa nchini.

"Bunyore katika mkoa wa Nyanza kuna mojawapo ya hali bora ya anga  ya kukuza bangi kwa sababu inakua kiasili. Nyamira Kisii na eneo la Mlima Kenya zitakuwa kipaumbele chetu kwa sababu tunataku kuinua Bunyore kuwa kaunti na huenda tutakuwa tunaagiza wakazi wa Bunyore kuwa na  bangi zao kuu," Alisema Wajackoyah.

Mgombea huyo wa urais pia alishikilia kuwa anapanga kufanya nchi ya Kenya kuwa nauchumi wa masaa 24.

"Wafanyikazi wawili wengine pia wataongezwa katika kila sekta ili tupatie Ijumaa kwa Waislamu na wale ambao wanataka kuangalia familia zao. Tutaeleza mengine zaidi," Alisema.

Aidha Wajackoyah aliwaonya raia wa kigeni wanaofanya kazi au kuwekeza hapa nchini dhidi ya kuchangia katika kuanguka kwa uchumi.